- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Lazima Tuitupilie Mbali Miungu ya Uongo na Miovu ya Utaifa na Ukabila Kwenye Jaa la Historia!
(Imetafsiriwa)
Kutokana na utaifa, ukabila na kuanzishwa kwa dola za kitaifa na mipaka yake katika ardhi za Waislamu, kitambulisho cha Waislamu kimeharibika na kutengana, ambapo Ummah wa Kiislamu hapo awali uliunganishwa katika udugu mmoja na ndani ya Dola moja ya Kiislamu, badala yake ukagawanyika katika dola za kitaifa zaidi ya 50 na vitambulisho vya kitaifa kufuatia kuvunjwa kwa Khilafah mnamo tarehe 28 Rajab, 1342, mikononi mwa Mustafa Kamal, “baba wa udhalifu”.
Hii ni licha ya ukweli kwamba utaifa na ukabila hudunishwa na kuchukiwa katika Uislamu na ambapo umoja katika aina zake zote lazima uwe chini ya uongozi mmoja wa Kiislamu kwa Waislamu.
Imepokewa na Abu Da’wud kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«لَيْسَ مِنَّا مَنْ دَعَا إِلَى عَصَبِيَّةٍ، وَلَيْسَ مِنَّا مَنْ قَاتَلَ عَلَى عَصَبِيَّةٍ، وَلَيْسَ مِنَّا مَنْ مَاتَ عَلَى عَصَبِيَّةٍ»
“Si miongoni mwetu anyealingania ‘Asabiyyah (utaifa/ukabila) au anayepigania ‘Asabiyyah au anayekufa kwa ajili ya ‘Asabiyyah.” Na katika hadith nyengine Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema kuhusu ukabila na utaifa, “Uacheni, hakika huo ni uvundo.” [Muslim na Bukhari].
Ibn Is-haq anasimulia, kwamba katika Khutba yake, Abu Bakr (ra) amesema, "وَإِنَّهُ لَا يَحِلُّ أَنْ يَكُونَ لِلْمُسْلِمِينَ أَمِيرَانِ؛ فَإِنَّهُ مَهْمَا يَكُنْ ذَلِكَ يَخْتَلِفْ أَمْرُهُمْ، وَأَحْكَامُهُمْ، وَتَتَفَرَّقْ جَمَاعَتُهُمْ، وَيَتَنَازَعُوا فِيمَا بَيْنَهُمْ، هُنَالِكَ تُتْرَكُ السُّنَّةُ، وَتَظْهَرُ الْبِدْعَةُ، وَتَعْظُمُ الْفِتْنَةُ، وَلَيْسَ لِأَحَدٍ عَلَى ذَلِكَ صَلَاحٌ" “Hakika hairuhusiwi kwa Waislamu kuwa na amiri wawili. Na pindi hilo likitokea, kutakuwa na hitilafu juu ya mambo na sheria zao, umma wa Waislamu utagawanyika na watagombana wao kwa wao. Hilo litasababisha kuachwa kwa Sunnah. Uzushi (bid’ah) utaonekana, mifarakano (fitnah) itaenea, ilhali hakuna chochote kati ya hayo kitakuwa ni maslahi.”
Cha kusikitisha ni kwamba, tunashuhudia hali ya ulimwengu wa Kiislamu leo kama ile ya Al-Aws na Al-Khazraj katika zama za ukabila na kutokuwepo utawala wa Uislamu. Kwa kiwango tunachoona fikra ya dola ya kitaifa, utaifa na ukabila zinaabudiwa kama sanamu za kisasa, kafara hutolewa kwa ajili yazo, wanaume na wanawake hufa na kuuawa kwa ajili yazo, na vita vinapiganwa katika utetezi wake. Leo, tunashuhudia migogoro ya kitaifa miongoni mwa Waislamu katika nchi kama Yemen, Pakistan-Afghanistan, Pakistan-Bangladesh na ndani ya Sudan. Mipaka ya kitaifa iliyochorwa na wakoloni ni mistari ya mgawanyiko kati ya jamii za Kiislamu, huku bendera za kitaifa zikipeperushwa kama nembo za ujinga juu ya mwili uliochanika wa Ummah.
Kwa hivyo, Waislamu hawasaidiani tena kutokana na mipaka hii ya kitaifa bali badala yake wanachukua msimamo wa kupooza wa kutoingilia kati. Kwa kiwango ambacho mauaji ya halaiki ya Waislamu huko Gaza na wavamizi haramu wa Kizayuni, mateso ya Waislamu wa Uyghur katika vituo vya mkusanyiko na Serikali ya China huko Xinjiang, au kuhamishwa na kuchinjwa kwa Waislamu wa Rohingya huko Myanmar, hayakuzuiwa wala kusimamishwa kutokana na mipaka hii ya dola za kitaifa.
Si tu ni makosa kuheshimu ‘masanamu’ haya ya kisasa bali pia ni wajibu kuyavunja na kuyaondoa katika uso wa dunia.
[أَتَتَّخِذُ أَصْنَامًا آلِهَةً إِنِّي أَرَاكَ وَقَوْمَكَ فِي ضَلاَلٍ مُّبِينٍ]
“Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi.” [Al-An’am: 74].
Mtume wa Uislamu (saw) alisimama kidete dhidi ya masanamu na imani za kijahiliya za zama zake, kamwe hakurudi nyuma. Viongozi wa washirikina wa Maqureish walipomsihi aache kuwatukana miungu yao na aache utume wake, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema, «لَوْ وَضَعُوا الشَّمْسَ فِي يَمِينِي وَالْقَمَرَ فِي شِمَالِي عَلَى أَنْ أَتْرُكَ هَذَا الْأَمْرَ حَتَّى يُظْهِرَهُ اللَّهُ أَوْ أَهْلِكَ فِيهِ مَا تَرَكْتُهُ» “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, hata kama wangeliweka jua kwa mkono wangu wa kulia, na mwezi katika mkono wangu wa kushoto, ili niwache amri hii (Uislamu) basi siiwachi mpaka Mwenyezi Mungu aidhihirishe au nife kwa njia hii.”
Kwa hivyo, ilikuwa ni mara tu Al-Aws na Al-Khazraj walipoacha ukabila na kuunusuru utawala wa Uislamu, ndipo wakawa nguvu moja dhidi ya nguvu za ukafiri. Ndani ya enzi ya Khilafah Rashida, Waislamu walizishinda dola kubwa, Warumi na Wafursi, na kisha wakawa dola inayoongoza duniani. Yote haya yanawasubiri Waislamu ikiwa wataachana na utaifa na ukabila, na kumteua Khalifa Rashid (khalifa muongofu) mmoja kwa Waislamu wote, kuanzia Indonesia hadi Morrocco.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema, «ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ» “…Kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume.” [Musnad Ahmad].
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Tsurroyya Amal Yasna
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir