Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Kenya

H.  24 Rajab 1441 Na: 1441/08 AH
M.  Alhamisi, 19 Machi 2020

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Mkurupuko wa Virusi vya Korona: Janga Jingine Linalo Fichua Madhara ya Urasimali na Tawala zake

Huku ulimwengu ukiendelea kukumbwa na janga la Virusi vya Korona, Kenya kama serikali nyingine duniani inaonekana kujikakamua na majaribio ya kukabiliana na janga hili. Visa saba vya maambukizi ya Virusi vya Korona visharipotiwa nchini japo hadi sasa hakuna vifo vyovyote.

Hizb ut-Tahrir Kenya ingependa kuangazia yafuatayo:

1- Mkurupuko wa maradhi ya Covid 19 unapata umakinifu mkubwa wa vyombo vya habari vya kiulimwengu huku habari nyingi zaidi juu ya janga hili zikionekana kukuza zaidi hofu na wasiwasi. Hata kama ni kweli kuwa dunia inakumbwa na janga la Virusi vya Korona, lakini muhimu hatupaswi kusahaulishwa mgogoro wa miaka takribani tisa sasa nchini Syria ambao ndio janga baya zaidi la kibinadamu ambapo takribani watu 700,000 wamelazimika kukimbia nyumba zao. Utawala wa Syria ukisaidiwa na Amerika na Urusi pamoja na mawakala wao wanatekeleza mauaji haya ambayo kwa sasa yamefanywa sio habari tena kwa vyombo vya habari!

2- Kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba, hivyo tunaunasihi mujtama kuchukua tahadhari za mapema kama vile kuosha mikono, na kujiepusha kuzuru maeneo ambayo kesi za maambukizi ya Virusi vya Korona zimeripotiwa. Uislamu umehimiza sana kuchukua hatua za mapema huku ukijenga zaidi fahamu ya mitihani ya Mwenyezi Mungu juu ya waja Wake yaani maambukizi kama haya yanapotokea yanapaswa kuchukuliwa kuwa ni mitihani na majaribio ya Mwenyezi Mungu ambayo hatimaye yaweza kuleta rehma kwa waliowema na adhabu kwa aliowataka Mwenyezi Mungu (swt).

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهَا أَنَّهَا «سَأَلَتْ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الطَّاعُونِ، فَأَخْبَرَهَا أَنَّهُ كَانَ عَذَابًا يَبْعَثُهُ اللهُ تَعَالَى عَلَى مَنْ يشَاءُ، فَجَعَلَهُ اللهُ تَعَالَى رَحْمَةً لِلْمُؤْمِنينَ، فَلَيْسَ مِنْ عَبْدٍ يَقَعُ فِي الطَّاعُونِ، فَيَمْكُثُ فِي بَلَدِهِ صَابرًا مُحْتَسِبًا يَعْلَمُ أَنَّهُ لَا يُصِيبُهُ إِلَّا مَا كَتَبَ اللهُ لَهُ إِلَّا كَانَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ الشَّهِيدِ

Imesimuliwa na Aisha (ra): “mke wa Mtume” kwamba alimuuliza Nabii wa Mwenyezi Mungu (saw) juu ya Tauni, Nabii wa Mwenyezi Mungu (saw) akamueleza kuwa, “Tauni ilikuwa ni adhabu ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa akiwapelekea wale awatakao, lakini Mwenyezi Mungu hufanya kuwa ni kheri kwa waumini.  Hakuna (miongoni mwa waumini) atakayebakia na kusubiri ndani ya ardhi ambayo kuna tauni ndani yake na kuzingatia kuwa hakuna litakalomfika isipokuwa lile aliloandikiwa na Mwenyezi Mungu, bali atalipwa ujira wake sawia na ule wa shahidi.” [Bukhari]

Ama kuhusu kuchukua tahadhari Mtume (saw) amesema:

إِذَا سَمِعْتُمْ بِالطَّاعُونِ بِأَرْضٍ فَلاَ تَدْخُلُوهَا، وَإِذَا وَقَعَ بِأَرْضٍ وَأَنْتُمْ بِهَا فَلاَ تَخْرُجُوا مِنْهَا

“Pindi mnaposikia mkurupuko wa maradhi ya tauni katika ardhi fulani, msiingie katika ardhi hiyo, na maradhi hayo yanapoingia katika ardhi mlioko ndani yake, basi msitoke”

3- Japo inaweza kusemwa kwamba kwa kuwa virusi hivi vimegunduliwa kwa mara ya kwanza itachukua miezi kadhaa kabla ya dawa yake kupatikana. Lakini ni muhimu kufahamu maumbile ya mfumo wa kirasilimali katika kutojali uhai wa wanadamu hivyo si la ajabu janga kama hili kugeuzwa na kuwa mradi wa kujitengezea mapato. Mtazamo wa kina juu ya viwanda vya kileo vya utengezaji madawa ni kuwa viwanda hivi vinasukumwa na kishajiisho kimoja pekee: kupata faida tu yaani upataji pesa kutokana na uzalishaji na uuzaji wa chanjo. Dawa za wagonjwa walio na maradhi sugu wanazozitumia kila siku zina faida zaidi hata kuliko chanjo ambayo hutoa athari ya tiba ya muda mrefu.

4- Kutingishika kwa uchumi wa mataifa mengi kutokana na mkurupuko wa Covid 19 hauonyeshi tu hali ya udhaifu wa tawala za kirasilimali bali pia udhaifu wa muundo wa kiuchumi wa kirasilimali ambao wenyewe huzalisha majanga. Kwa hakika ni mithili ya nyumba ya buibui nyumba iliyoduni zaidi kuliko zote! Hili lapaswa kufungua macho ya wasomi ili wafanye kazi ya kuleta mabadiliko halisi ya kimfumo kupitia kuung'oa urasilimali na kuubadilisha kwa Uislamu ulio na nidhamu imara ya kiuchumi.

5- Ummah wa Kiislamu, pindi unapokabiliana na janga hili, unapaswa kulikabili kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu sambamba na kuchukua hatua za kujikinga na kujitibu. Kumtegemea Mwenyezi Mungu (Tawakkul) ni mojawapo ya sifa njema za Waislamu inayowafanya wasiogope chochote ila Mwenyezi Mungu kwani daima huweka tegemeo lao kwake Yeye Aishiye milele.

6-Kwa kuendelea kwa teknolojia ya kisasa, dola ya Khilafah itaweza kuweka mazingira ambayo utafiti na ufanisi vitanawiri. Ufadhili wa utafiti waweza kutengewa viwanda vya utengenezaji madawa ili vitengeze na kutafiti chanjo na madawa kwa ajili ya matibabu. Al-Khilafah itawekeza sana katika sekta ya madawa sio kama fadhila kwa raia wake au kama pato lenye faida bali kama jukumu la dola katika kutimiza mahitaji ya umma ambayo hujumuisha usalama na afya. Mtume (saw) amesema katika hadithi iliyo simuliwa na Ubaidullah bin Mihswan Al-Ansaariy:

من أصبح منكم آمنا في سربه، معافى في جسده، عنده قوت يومه، فكأنما حيزت له الدنيا بحذافيرها‏

“Yeyote atakayeianza siku kwa kuhisi usalama na afya njema kwa familia, na mwenye kumiliki mahitaji yake ya siku, ni kama ambaye ni aliyekusanyiwa dunia yote.” (Tirmidhi)

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Kenya
Address & Website
Tel:  +254 707458907
E-Mail: mediarep@hizb.or.ke

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu