Afisi ya Habari
Wilayah Misri
H. 11 Muharram 1447 | Na: 1447/01 |
M. Jumapili, 06 Julai 2025 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Ajali za Barabarani nchini Misri: Ushahidi Tosha wa Kukosekana kwa Ustawi wa Jamii na Ufisadi wa Mfumo wa Kirasilimali
(Imetafsiriwa)
Katika tukio ambalo limekuwa la kusikitisha, watu waliamka siku chache zilizopita na kushuhudia maafa mengine ambayo yalisababisha vifo vya watu tisa wasio na hatia katika ajali iliyotokea kwenye Barabara ya Kanda katika Jimbo la Monufia, chini ya wiki moja baada ya maafa ya kuhuzunisha ambapo wasichana wachanga kumi na nane waliangamia katika ajali sawia, ikitofautiana na ile ya awali tu na kwa idadi ya wahasiriwa. Barabara ya Kanda - ambayo serikali imekuwa ikiitangaza kwa muda mrefu kama "mafanikio ya kitaifa" - imekuwa shahidi wa kudumu wa upuuzi wa yale yanayodaiwa kuwa mafanikio yanayosifiwa na watawala huku wakijificha nyuma ya mabango ya vyombo vya habari vya uwongo na kupuuza haki msingi ya watu: kuishi kwa usalama kwenye barabara ambazo hazinyakui maisha yao.
Misiba hii si ajali za nasibu ambazo wengine hutoa hoja ya majaaliwa au bahati mbaya. Bali ni matokeo ya kimaumbile na ya moja kwa moja ya kukosekana kwa uangalizi wa kweli kwa mambo ya watu na ufisadi wa kudumu uliokita mizizi katika vyombo vya dola - ufisadi uliokita mizizi katika kutabaniwa kwa mfumo mbovu wa kibepari unaopima mambo kwa kiwango cha matumizi na kuyapima katika mizani ya faida na hasara, sio kwa mizani ya haki na wajibu, bila kuzingatia yale ambayo Mwenyezi Mungu ameyahalalisha au kuyaharamisha.
Ripoti ya Shirika la Habari la Associated Press ya tarehe 27 Juni 2025 ilieleza wazi kwamba lori lililogharimu maisha ya watu kumi na tisa, miongoni mwao wakiwa wasichana wadogo kumi na nane katika pindi cha ujana wao, lilikuwa likisafiri kwa mwendo wa kasi kupita kiasi na kwamba barabara mbovu ilikuwa ikifanyiwa ukarabati ambao haujakamilika. Hata hivyo, mamlaka iliruhusu magari kusafiri juu yake bila udhibiti au hatua za usalama. Katika ripoti nyingine ya shirika hilo ya tarehe 5 Julai 2025 kuhusu ajali ya mabasi mawili ya abiria katika Barabara ya Kanda, ilibainika kuwa upakiaji kupita kiasi, kushindwa kwa madereva kuzingatia viwango vya mwendo kasi, na uzembe wa taa na alama za barabarani vyote hivyo ni sababu za moja kwa moja za mauaji hayo. Badala ya kuviwajibisha vyombo vya dola kwa kushindwa kwao kutunza na kulinda barabara na kufuatilia madereva, wenye mamlaka walikimbilia kuzima hasira za wananchi kwa fidia ndogo ndogo na kauli tupu za “huzuni kubwa” na “hatua za dharura,” kana kwamba tatizo linatokana na ukosefu wa uombolezaji, na sio kukosekana uangalizi!
Kuhifadhi maisha ni miongoni mwa malengo makubwa ya Uislamu, ambao umeyafanya kuwa ni jukumu la mtawala kusimamia maslahi ya watu na kulinda haki zao - kutojishughulisha na kupotosha ufahamu wao na kuwahadaa kwa miradi ambayo uso wake ni mng'aro wa kirongo na ambayo msingi wake ni uzembe. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «وَالْإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ» “Imam ni mchunga na anawajibika kwa raia wake.”
Jukumu hili linatimizwa tu kwa kuasisi mfumo wa utawala unaodhibiti mambo ya maisha kwa vipimo vya Shariah, si kwa vipimo vya soko na faida.
Barabara hizi na huduma za umma ni mali ya umma ambayo jamii ya watu hunufaika nayo, na serikali inalazimika kuzitunza na kuhakikisha usalama wa watu juu yao bila uzembe. Tunachokiona leo cha Barabara ya Kanda na barabara nyenginezo kukosa miundombinu ya kimsingi - licha ya kuwa njia kuu ya makumi ya maelfu ya wafanyikazi na masikini - ni matokeo ya ufisadi uliokita mizizi katika muundo wa mfumo wa kibepari unaowaona wanadamu kuwa idadi tu katika orodha ya faida.
Kwa mujibu wa ripoti za Wizara ya Afya na Idadi ya Watu na ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa, Misri imeshuhudia vifo vya zaidi ya watu 7,000 kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, idadi ambayo inazidi majeruhi wa migogoro mingi ya kivita. Hasa, vingi vimejikita kwenye barabara mpya zilizojengwa kama vile Barabara ya Kanda, Barabara kuu ya Misri, na Barabara ya Alamein. Hii inadhihirisha kuwa majanga haya hayatokani na barabara za zamani bali ni fikra ya kusimamia fedha za umma ambayo haijali usalama wa watu. Mfumo wa kibepari, ambao unahalalisha ubinafsishaji na uuzaji wa mali na kuifanya miundombinu kuwa njia ya kukusanya faida, hauwezi kutoa uangalizi wa kweli, kwa kuwa inauona kuwa mzigo wa kifedha, sio haki ya Shariah.
Uislamu unamwona mwanadamu kama kiumbe anayekirimiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Unaona kuhifadhi maisha, mali, na heshima yake kuwa lengo ndani yake wenyewe na unawajibisha dola kuhakikisha kila kitu kinachohitajika kwa hilo. Chini ya Dola ya Kiislamu, barabara hudumishwa na kuwekewa viwango muhimu vya usalama - mwangaza wa kutosha, vikomo vya kasi vinavyofaa, ukaguzi wa mizigo, vikomo vya nyakati, vizuizi, na kutekeleza adhabu za kukomesha za Shariah kwa wale wanaohatarisha maisha bila kujali. Dola ya Kiislamu inajilazimisha kutenga fedha zinazohitajika ili kutunza barabara, si kama fadhila bali kama wajibu wa Shariah.
Yaliyotokea katika maafa ya wasichana 18 na maafa ya wahasiriwa 9 ni ukurasa tu kutoka kwa rekodi ndefu iliyoandikwa kwa miaka chini ya mfumo unaojali tu maslahi ya wenye ushawishi na akaunti zao za benki. Na wakati wengine wanasema hizi "ajali zimejaaliwa," Shariah inatufundisha kwamba jaala haiondoi jukumu. Kwa hakika, kutelekeza hatua za Shariah za kuwalinda watu ni uzembe ambao unalazimu uwajibikaji. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
[وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ إِنَّ اللَّهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا]
“Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni.” [An-Nisaa: 29].
Basi vipi kuhusu mfumo unaoacha mamia ya maisha ya watu wakichukuliwa kwenye lami kila mwaka na kutoa tu taarifa ya rambirambi au fidia kidogo tu?
Tiba ya maafa haya haiko katika kauli za kulaani au ahadi za marekebisho, bali ni katika kuweka mfumo unaotawala kwa mujibu wa Shariah na unaochunga mambo ya watu kwa mujibu wa hukmu zake - kukata mikono ya mafisadi na kudhibiti vitendo vyake kwa kipimo cha halali na haramu, sio kwa kipimo cha "mregesho wa uwekezaji"! Mfumo huu wa kibepari, ambao umefeli kuwaokoa watu kutokana na umasikini wao, magonjwa, na majanga ya barabarani, ni mfumo ule ule unaotia mizizi ufisadi, unapinga Uislamu, na unazuia kusimamishwa kwa Khilafah, ambayo peke yake ina uwezo wa kuyafanya maisha ya watu na utu kuwa kipaumbele, na sio chombo cha propaganda.
Leo, Umma wa Kiislamu unakabiliwa na chaguo la wazi: ima kubaki mateka wa mfumo wa kibepari unaoua watoto wao barabarani, kuwaua kwa njaa majumbani mwao, na kuwahadaa kwa kauli mbiu za uwongo, au kusonga ili kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume inayotabikisha hukmu ya Mwenyezi Mungu na kuwarudishia watu haki yao ya maisha salama na yenye staha.
Nafsi hizi zinazochukuliwa kila siku katika barabara za Misri na katika ardhi zote za Waislamu ni mashahidi wa ukweli wa kauli yetu kwamba hakuna wokovu kwa Ummah isipokuwa katika Uislamu kama mfumo, utawala, na uongozi. Damu hizi safi ni mwito kwa kila ambaye bado ana chembe ya imani ndani ya moyo wake wa kusonga ili kusimamisha Dola ya haki na uadilifu, ili Ummah upate kuhukumiwa tena na yale yote aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kuvunja minyororo ya utiifu, ufisadi, na uzembe.
[الَّذِينَ إِنْ مَكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ وَلِلَّهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ]
“Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.” [Al-Hajj: 41]
Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Misri
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Misri |
Address & Website Tel: http://hizb.net/ |
E-Mail: info@hizb.net |