Afisi ya Habari
Wilayah Uturuki
H. 20 Rabi' I 1445 | Na: 1445 / 02 |
M. Alhamisi, 05 Oktoba 2023 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Uchumi Unaotegemea Riba Huzua Matatizo, Sio Suluhisho
(Imetafsiriwa)
Hafiza Ghaya Arkan, mkuu wa Benki Kuu, alisema katika uwasilishaji wake mbele ya Kamati ya Mipango na Bajeti ya Bunge Kuu la Ututuki mnamo Jumanne, Oktoba 3, kwamba mwaka ujao utashuhudia kupungua kwa mfumko wa bei. Mfumko wa bei wa kila mwaka unatarajiwa kupungua baada ya Mei 2024, na kufikia tarakimu moja ifikapo 2026. Akijibu maswali kuhusu gharama ya mfumo wa kuhifadhi fedha za kigeni, Arkan alisema kuwa Benki Kuu imelipa lira za Kituruki bilioni 70 kama sehemu ya ulinzi wa amana na malipo ya kiwango cha ubadilishaji mwaka wa 2022. Walipiga hesabu malipo yaliyolipwa katika nusu ya kwanza ya 2023 kuwa lira za Uturuki bilioni 90. Taarifa za Arkan zinaonyesha kuwa lira za Kituruki bilioni 90 zitalipwa kwa amana zilizohifadhiwa na kiwango cha ubadilishaji wa fedha kutoka Hazina katika nusu ya pili ya mwaka huu. Kwa hivyo, utekelezaji wa amana zilizolindwa kwa kiwango cha ubadilishaji umeweka mzigo mpya wa lira za Kituruki bilioni 250 kwa watu ambao tayari wanang’ang’ana.
Madhumuni ya awali ya mfumo wa amana unaolindwa na viwango vya ubadilishaji, uliotangazwa na Rais Erdogan karibu miaka miwili iliyopita mnamo Disemba 21, 2021, kama njia ya uokoaji ili kuondokana na mzozo huo, ilikuwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni, kuzuia mashambulizi kwa kiwango cha ubadilishaji, na kuongeza thamani ya Lira ya Uturuki. Hata hivyo, hili halijaafikiwa, na sasa masuluhisho mapya yanatafutwa ili kupunguza mzigo wa amana zinazolindwa na kiwango cha ubadilishaji fedha kwenye Hazina. Kwa bahati mbaya, serikali kwa mara nyingine tena inatoa sera ambazo zimejaribiwa mara nyingi huko nyuma na zimetoa matokeo mabaya. Taratibu hizi, zinazotekelezwa pamoja na sera ngumu ya fedha, hazitaboresha hali ya wastaafu wanaotatizika kupata riziki, wafanyikazi wanaojaribu kujikimu kima cha chini cha mishahara, wakulima wasioweza kupata fidia ya haki kwa mazao yao, na wafanyibiashara kupondwa chini ya mzigo wa kodi. Kwa kuwa ongezeko la ushuru husababisha mfumko wa bei, uwezo wa ununuzi wa watu unapungua siku baada ya siku. Kwa hivyo, hatua zote hizi hazikuchukuliwa ili kuongeza ustawi wa watu, lakini, kinyume chake, kuongeza imani ya mtaji wa kigeni, kuongeza kiwango cha mkopo cha Uturuki, kupunguza malipo ya hatari ya deni, na kurefusha uhai wa mfumo wa uchumi wa kibepari kwa jumla.
Iwapo serikali inawajali wananchi kwa dhati na kuwa na nia ya dhati katika kuboresha maisha yao, ingekubali kwamba sababu ya kweli ya mfumko wa bei na mtikisiko wa uchumi ni mfumo wa pesa zisizo na thamani ya dhati (fiat) unaozingatia dolari, na ingefafanua kuwa tatizo ni mfumo wa uchumi wa kibepari wenyewe, ambao hustawi kwa riba na kodi kubwa. Rais Erdogan aliposema, "Kama Muislamu, nitaendelea kufanya kile ambacho dini yetu inatuambia. Hii ndiyo amri," alipaswa kurudi kwenye mfumo wa uchumi wa Kiislamu. Hata hivyo, alifanya kinyume chake kwa kuweka gharama ya riba ya amana iliyolindwa kwa kiwango cha ubadilishanaji fedha kwa wananchi ambao tayari wameshalemewa. Ijapokuwa tumesema kuwa suluhisho lipo katika mfumo wa uchumi wa Kiislamu, hatamu za uongozi zimekabidhiwa kwa wanauchumi wa kibepari.
Katika mfumo wa uchumi wa Kiislamu, sarafu inaegemezwa kwa dhahabu na fedha. Kwa sababu ya thamani ya asili ya dhahabu, hakuna upotevu wowote wa thamani ya pesa. Kwa kudumisha thamani ya pesa, utulivu wa bei unahakikishwa, na mfumko wa bei unazuiwa. Katika mfumo wa uchumi wa Kiislamu, hakuna nafasi kwa riba, na pesa kamwe haziruhusiwi kufanyiwa biashara katika maeneo yaliyoharamishwa, kama vile benki za riba na soko la hisa. Hii inaruhusu fedha kuingia sokoni, biashara kustawi, uzalishaji kuongezeka, na mfumko wa bei kupungua kabisa. Kwa hivyo, kinachotakiwa kufanywa leo si kufanya mabadiliko katika sera zinazohujumu mfumo wa uchumi wa kibepari bali ni kuanzisha kampeni ya kina dhidi ya mfumo wa kibepari wa kilimwengu kwa ajili ya kutabikisha mfumo wa uchumi wa Kiislamu. Hili ni jukumu la watawala pamoja na Waislamu wanaopaswa kuwahisabu watawala. Hatua nyengine zozote kando na hizi hazitasuluhisha matatizo na zitapelekea masikitiko kesho Akhera. Kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
[وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَع۪يشَةً ضَنْكاً وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيامَةِ أَعْمَى]
“Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.” [Surat Ta-Ha:124].
Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir katika Wilayah Uturuki
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Uturuki |
Address & Website Tel: |