Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Erdogan asema Neno la Kweli kuhusu Riba ambalo kwalo Unakusudiwa Urongo

(Imetafsiriwa)

Habari:

Kushuka thamani kwa lira ya Uturuki.

Maoni:

Sarafu ya taifa ya Uturuki, lira ya Uturuki, imeporomoka sana katika robo ya mwisho ya mwaka huu, kutoka lira 8.86 za Uturuki kwa dolari moja mwezi Oktoba hadi lira 16.42 za Uturuki kwa dolari moja ya Marekani. Kwa hivyo, lira ya Uturuki ilipoteza takriban maradufu ya thamani yake dhidi ya dolari ya Marekani na hiyo ni ndani ya kipindi cha miezi kadhaa. Sababu kuu ya kushuka kwa thamani ya sarafu yake ni kutokana na deni kubwa la nje na riba yake ambayo Uturuki haina uwezo wa kuilipa kwa wakati. Wizara ya Fedha ya Uturuki ilitangaza mwezi huu wa Machi kuwa deni kuu ni dolari bilioni 262.1 lakini lilifikia dolari bilioni 448.4 kwa sababu ya riba na ada za dhamana kwa madeni. Hili ni ongezeko la karibu mara mbili ya deni. Kando na hayo, madeni ya dharura ambayo Uturuki inapaswa kulipa kwa mwaka mmoja tu yamefikia dolari bilioni 168.7. Mpaka sasa Uturuki haina uwezo wa kulipa hata madeni ya haraka kwa fedha za kigeni. Nakisi hii itajumuishwa kimuundo katika ulipaji ujao ambao utaiingiza Uturuki katika janga la madeni linalozidi kukua. Hili miongoni mwa mambo mengine yamesababisha ukosefu wa imani katika lira ya Uturuki ambayo ilisababisha uwekezaji wa fedha za kigeni badala ya lira ya Uturuki, ambayo ilizidisha kushuka kwa thamani ya lira ya Uturuki zaidi.

Rais Recep Tayyip Erdogan, hata hivyo alidai kuwa sababu ya kushuka kwa thamani ya sarafu hiyo ilitokana na ghiliba za mataifa ya kigeni katika soko la fedha na kwamba Uturuki iko katikati ya "vita vya uhuru wa kiuchumi". Alikataa kuongeza kiwango cha riba ili kupunguza mfumko wa bei unaokwenda kinyume na nadharia ya msingi ya Uchumi wa Kirasilimali ambayo anaitekeleza. Alisema, "Hatutaliponda taifa letu kwa riba" na akasema kwamba hatafuatana na wale wanaounga mkono riba. Pia alisema, “Suala hili si suala la kawaida, marafiki zetu wana nini kwamba wanakuwa watetezi wa riba. Maadamu ningalipo madarakani, samahani, nitaendelea na mapambano yangu dhidi ya riba hadi mwisho, na mapambano yangu dhidi ya mfumko wa bei hadi mwisho.” Hata alilitilia nguvu hili kwa mafundisho ya Kiislamu na akasema: “Ni nini? Tunapunguza viwango vya riba. Msitarajie kitu chengine chochote kutoka kwangu." "Kama Muislamu, nitaendelea kufanya kile kinachotakiwa na nas (akikusudia uharamu wa riba katika nususi za Kiislamu)."

Wiki hii, lira ya Uturuki ilipata nafuu kidogo baada ya ahadi zilizotolewa na Rais Erdogan kwamba atafidia akiba ya raia kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha. Hili kwa kiasi fulani liliongeza imani ya watu kwa lira ya Uturuki na wakaanza kubadilishana dolari kwa Lira ya Uturuki. Hii ina maana kwamba watu wameshajiishwa kujihusisha na uwekaji akiba kwa msingi wa riba lakini kwa sharti iwe kwa msingi wa Lira ya Uturuki pekee. Serikali kisha itakuwa kama mdhamini wa nakisi ambayo inasababishwa na kushuka kwa thamani ya sarafu. Kwa hivyo, kwa hakika hii ina maana kwamba mtu au kampuni ambayo ina lira milioni moja za Kituruki kwenye akaunti yake ya akiba itapata lira za Kituruki milioni mbili mwaka mmoja baadaye endapo dolari itakuwa na nguvu mara mbili dhidi ya lira katika mwaka mmoja. Kwa maana nyengine: serikali italipa riba zaidi.

Kwa hiyo, iko wapi "nas" ambayo Erdogan anaizungumza sasa? Je, katazo la Kiislamu la riba ni halali kwa dolari za Marekani pekee na si kwa lira za Uturuki? Kwa miaka 20 iliyopita jamii imekuwa na ari ya kujiingiza katika mikopo yenye riba kupitia benki za serikali na mikopo iliyofadhiliwa na serikali ambapo kila aina ya miamala yenye riba imekuwa ikiruhusiwa katika utawala wake wote. Wengi wa jamii ya Kituruki ni wadaiwa wa riba na wanashajiishwa kuendelea maadamu wanawekeza kwa lira. Hii inafanya msimamo wake dhidi ya riba na mwonekano wake katika miaka ya hivi karibuni usiwe wa kuaminika sana. Uwezekano mkubwa zaidi, yeye hutumia hii kama kisingizio kilichofinikwa kulaumu hali mbaya ya uchumi na kukwepa majukumu yake. Hadi sasa kuhusu na "nas" inayohusiana na riba. Ziko wapi "nas" nyengine za kupangilia jamii nzima? Au hakuna "nas" yoyote aliyokuja kuipangilia? Kama vile "nas" inayohusiana na pombe, ukahaba, kanuni ya mavazi, udhibiti wa jinsia, elimu, fedha, mahusiano na mataifa mengine, utawala nk...

Kwa hivyo, mpango wa utekelezaji uliojengwa juu ya msingi wa riba ambapo serikali itakuwa kama mdhamini wa nakisi inayosababishwa na kushuka kwa thamani ya sarafu hauendi tu kinyume na mafundisho ya Kiislamu lakini pia ni suluhisho la kirongo ambalo litauweka mfumo mbovu hai. Hii ni kwa sababu, ili kutekeleza mpango huu wa fidia ya fedha, serikali inahitaji pesa ambazo haina. Haina uwezo wa kulipa hata riba ya madeni yake, itawezaje kumudu fidia kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha? Hii ina maana kwamba serikali itachukua mikopo yenye riba zaidi na kuongeza madeni yake ya nje hata zaidi, wakati madeni haya yenye riba ndiyo yaliyokuwa sababu ya awali ya majanga yake ya kifedha. Pia, haitaweza kuyalipa, ambapo itasababisha msururu wa madeni ya milele na fursa kwa dola za kikoloni kuimarisha utawala wao hata zaidi.

Suluhisho pekee la migogoro ya fedha nchini Uturuki sio Urasilimali zaidi au demokrasia zaidi bali ni kusimamishwa kwa Uislamu na Dola ya Khilafah  kwa njia ya Utume.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Okay Pala

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Uholanzi

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu