- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa
Amiri wa Hizb ut Tahrir
Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook
Jibu la Swali:
Sisi Hatusemi kuwa Habari ya Upokezi wa Mmoja Mmoja (Khabar Ahaad) Ikataliwe, Bali Tunasema Yalazimu Kufanyiwa Kazi
Kwa: Anis Merji
Swali:
Assalam Aleykum
Hadithi kubwa zaidi katika Aqida ni Hadith Ahaad, nayo ni Hadith ambayo Jibril alikuja kumuuliza maswali Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ambapo Mtume alisema: Je, munamjua muulizaji ni nani? Wakasema Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajua zaidi. Akasema: Huyu ni Jibril amekuja kukufunzeni Dini yenu. Hii ni khabar ahaad katika Aqida, basi ni kwa nini tunaikataa?
Jibu:
Waaleykum Salaam wa Rahmatullah wa Barakatuh,
Kwanza: Inaelekea hukulidiriki jibu tulilolitoa tarehe 10/09/2022 M kuhusu kuichukulia Hadith kuwa ni dalili katika hukmu za kisharia.Yaani hakulidiriki katika sura yake, sisi hatusemi kuwa khabar ahaad ikataliwe, bali twasema kuwa khabar ahaad ni wajibu kufanyiwa kazi kwayo, lakini haihisabiwi kama dalili ya kukatikiwa katika Aqida, yaani hadith ahaad haitumiwi kama dalili katika Aqida kwa sababu hadith ahaad ni dhanni... Kutochukua Aqida kwa dhana si uzushi, bali iko ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwani ziko Aya nyingi ndani yake Mwenyezi Mungu anawakemea wale wanaoamini kwa dhana. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: ﴿إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمْ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ بِهَا مِنْ سُلْطَانٍ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَمَا تَهْوَى الْأَنْفُسُ وَلَقَدْ جَاءَهُمْ مِنْ رَبِّهِمُ الْهُدَى﴾ “Hayo hayakuwa ila ni majina mliyo wapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo. Hawafuati ila dhana tu na kipendacho nafsi. Na kwa yakini uwongofu ulikwisha wafikia kutoka kwa Mola wao Mlezi.” [An-Najm: 23] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: ﴿إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ لَيُسَمُّونَ الْمَلَائِكَةَ تَسْمِيَةَ الْأُنْثَى * وَمَا لَهُمْ بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئاً﴾ “Hakika wasio amini Akhera bila ya shaka wao ndio wanawaita Malaika kwa majina ya kike. Nao hawana ujuzi wowote kwa hayo isipo kuwa wanafuata dhana tu. Na dhana haisaidii chochote mbele ya haki.” [An-Najm: 27-28] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: ﴿وَمَا يَتَّبِعُ أَكْثَرُهُمْ إِلَّا ظَنّاً إِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئاً﴾ “Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai kitu mbele ya haki.” [Yunus: 36] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: ﴿الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ كَبُرَ مَقْتاً عِنْدَ اللَّهِ وَعِنْدَ الَّذِينَ آمَنُوا﴾ “Hao ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu pasipo ushahidi wowote ulio wafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walio amini.” [Al-Ghaafir: 35] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: ﴿وَكَيْفَ أَخَافُ مَا أَشْرَكْتُمْ وَلَا تَخَافُونَ أَنَّكُمْ أَشْرَكْتُمْ بِاللَّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَاناً﴾ “Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia uthibitisho.” [Al-An’am: 81] na aya zengine nyingi…
Aya hizi ziko wazi katika kuwashutumu wale wanaofuata dhana, na katika kuwashutumu wale wanaofuata bila ya ubainifu, yaani bila ya dalili ya kukatikiwa, na kukemewa kwao na kukashifiwa kwao ni dalili ya katazo la kukatikiwa la kufuata dhana, na katazo la kukatikiwa la kufuata yale ambayo hayakujengwa juu ya dalili ya kukatikiwa... Na kwa sababu aya hizi zimefungika katika masuala ya Aqida, ni makhsusi kwa Aqida... Na yote haya yanaashiria maana ya kukatikiwa kwamba masuala ya Aqida ni lazima yasimame juu yake dalili ya kukatikiwa, vyenginevyo hayazingatiwi, na kwamba haijuzu dalili yake kuwa ya dhana.
Pili: wajibu wa kusimamisha dalili ya kukatikiwa juu ya Aqida ili iwe ni Aqida, na hilo linaashiriwa na Aya zenye hoja zilizo wazi... Hili ni kuhusiana na Aqida.
Ama hukmu za kisheria, inajuzu dalili yake kuwa dhanni, na wala sio sharti kuwa ya kukatikiwa, bali inaweza kuwa dhanni, kwani imethibitika katika andiko la Qur'an Tukufu kwamba inaweza kuhukumiwa kwa ushahidi wa mashahidi wawili, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alihukumu kwa ushahidi wa shahidi mmoja na kiapo cha mwenye haki, na akakubali ushahidi wa mwanamke mmoja katika kunyonyesha, haya yote ni khabar ahaad, na hukmu ni ulazimishaji, na ulazimishaji huu si chochote ila ni ufanyiaji kazi khabar ahaad. Na kuitumia khabar ahaad kama dalili katika kutoa hukmu kama vile kukubali ushahidi na kuhukumu kwa mujibu wake, na yote haya ni katika vitendo, yaani katika hukmu ya Sharia. Na Maswahaba, Mwenyezi Mungu awawie radhi, walikuwa wakikubali maneno ya Mjumbe mmoja katika kuwapa habari kuhusu hukmu ya sharia
kama suala la kuelekea Al-Kaaba (katika swala). Imepokewa na Muslim aliyesema: ametuhadhithia Abdulrahman bin Yusuf aliyesema ametupa habari Malik bin Anas kutoka kwa Abdillah bin Dinar kutoka kwa Abdullah bin Umar amesema: : بَيْنَا النَّاسُ بِقُبَاءٍ فِي صَلَاةِ الصُّبْحِ إِذْ جَاءَهُمْ آتٍ فَقَالَ: إِنَّ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ قَدْ أُنْزِلَ عَلَيْهِ اللَّيْلَةَ قُرْآنٌ، وَقَدْ أُمِرَ أَنْ يَسْتَقْبِلَ الْكَعْبَةَ فَاسْتَقْبِلُوهَا، وَكَانَتْ وُجُوهُهُمْ إِلَى الشَّأْمِ، فَاسْتَدَارُوا إِلَى الْكَعْبَةِ.. “Pindi watu walipokuwa katika swala ya asubuhi alikuja my akasema: hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) imemteremkia Quran usiku huu, na ameamrishwa kuelekea Al-Kaaba (katika swala) basi wakaielekea, na nyuso zao zilikuwa zinaelekea Ash-Sham, basi wakaigeukia Al-Kaaba…”
Na vilevile suala la kuharamishwa pombe, amepokea Al-Bukhari akisema:
Ametuhadithia Yakub bin Ibrahim ametuhadithia Ibn ‘Ulayyah ametuhadithia Abdulaziz bin Suhaib amesema: amesema Anas bin Malik (ra): مَا كَانَ لَنَا خَمْرٌ غَيْرُ فَضِيخِكُمْ هَذَا الَّذِي تُسَمُّونَهُ الْفَضِيخَ، فَإِنِّي لَقَائِمٌ أَسْقِي أَبَا طَلْحَةَ وَفُلَاناً وَفُلَاناً إِذْ جَاءَ رَجُلٌ فَقَالَ: وَهَلْ بَلَغَكُمْ الْخَبَرُ؟ فَقَالُوا: وَمَا ذَاكَ؟ قَالَ: حُرِّمَتْ الْخَمْرُ. قَالُوا: أَهْرِقْ هَذِهِ الْقِلَالَ يَا أَنَسُ. قَالَ: فَمَا سَأَلُوا عَنْهَا وَلَا رَاجَعُوهَا بَعْدَ خَبَرِ الرَّجُلِ). “Sisi hatukuwa pombe, isipokuwa hii munayoiita al-Fadhikh, na mimi nilikuwa nimesimama namnyesha Abu Talha na fulani na fulani. Akaja mtu akasema: je, imekufikieni habari? Wakasema: Ni nini hiyo? Akasema: Pombe imeharamishwa. Wakasema: Tupa madebe haya ewe Anas. Akasema: Basi hawakuuliza juu yake, wala hawakushauriana baada ya kuambiwa na mtu huyo.”
Yote haya hayafanyi kuwepo na shaka yoyote kwamba dalili dhanni inaweza kutumiwa kama dalili katika hukmu ya Sharia.
Hakika miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu juu yetu ni kwamba ametukataza kuichukua Aqida kwa dhana na akaifanya iwe kwa dalili ya kukatikiwa ili Umma ujumuike pamoja juu yake bila ya kukhitilafiana, kwa hayo Aqida itakuwa safi na takatifu bila ya Muislamu kumkufurisha ndugu yake Muislamu kwa sababu ya kutofautiana kwao katika Hadith dhanni katika Aqida, kwa sababu ikhtilafu katika Aqida ni njia ya kufikia ukafiri, tofauti na hukmu ya Kisharia inayotokana na Hadith ahaad. Ikhtilafu katika hukmu ya Kisharia kihakika sio njia ya kupeleka katika ukafiri. Yeyote anayesema kuwa upanzi shirika (Al-Muzaara’ah) unaruhusiwa kwa sababu ana Hadith ahaad sahih, haimfanyi kuwa kafiri yule anayesema kuwa upanzi shirika ni haramu kwa sababu ana hadith ahaad sahih, na kadhalika... na kwa mlango huu yajuzu kuifanyia kazi hadith ya kukatikiwa na dhanni katika hukmu ya Kisharia na kutochukua hadith dhanni katika Aqida kwa sababu masuala ya Aqida huchukuliwa kutoka kwa yakini.
Pili: Kisha, kutochukua Hadith ahaad katika masuala ya Aqida kulisemwa na magwiji wa wanazuoni wa fiqhi (Fuqaha), kama Imam Abd al-Rahim bin al-Hasan bin Ali al-Asnawi al-Shafi'i, Abu Muhammad, Jamal al-Din. “aliyefariki mwaka 772 H” ametaja katika kitabu chake “Nihaayat al-Sul Sharh Minhaj al-Wasul”: (Na jua kwamba udhihirisho wa dalili ndio njia ya kutokea katika kanuni nyingi za fiqhi, kama vile maelezo ya jumla, khabar ahaad, mlinganisho (qiyas) na ufuatanishi (al-Istaishab), na kadhalika. Wanazuoni wa Usul al-Fiqh, hata wakikubali kufanya kazi nazo, hizo kwao wao sio dalili za fiqhi, bali ni ishara (Amaraat) juu yake. Dalili kwao haitoki isipokuwa kwa lile ilokatikiwa kwayo), wanazuoni wa usul hawazichukulii kuwa ni dalili za fiqhi yaani dalili za hukmu za kisharia kuwa ni dalili, bali wanazichukulia kuwa ni ishara juu ya hukmu za Kisharia, na hiyo ni kwa sababu dalili dhanni hawaichukulii kuwa ni dalili kwao, bali wanaichukulia kuwa ni ishara (Amaarah), kwani dalili kwao haitoki isipokuwa kwa ile iliyokatikiwa kwayo. Hivyo dalili za misingi ya dini lazima ziwe za kukatikiwa (qat’i), na hivi ndivyo alivyosema Ibrahim bin Musa bin Muhammad al-Lakhmi al-Gharnati, maarufu kama al-Shaatibi “aliyekufa: 790 H” katika kitabu chake “Al-Muwaafaqaat”: (Misingi ya fiqhi katika dini ni ya kukatikiwa, si dhanni, na dalili ya hilo ni kwamba inaregea katika ujumla wa Sharia, na kwa sababu ya hivyo, ni ya kukatikiwa... Na lau ingejuzu kuifanya dhanni kuwa asili, katika misingi ya fiqhi, ingejuzu kuifanya kuwa asili katika misingi ya dini, na sio hivyo kwa itifaki. Na vilevile hapa, kwa sababu uwiano wa misingi ya fiqhi na Sharia ni kama uwiano wa msingi ya dini), kwa hivyo anatumia hoja kuwa misingi ya fiqhi ni ya kukatikiwa qat’i), kutokana na umbile lake kama misingi ya dini, na misingi ya dini kwa makubaliano ni ya kukatikiwa (qat’i) , na misingi ya dini ni chimbuko lake ni Aqida, na Aqida ndiyo misingi ya dini... nk
Tatu: Hata hivyo, kuna jambo ambalo ni lazima litiliwe mkazo, nalo ni kwamba maana ya kutoitakidi kwa dalili dhanni haimaanishi kukataa yaliyomo ndani ya Hadith hizi na kutosadikisha yale yaliyokuja ndani yake, bali ni kutoyachukua katika Aqida ambapo Muislamu anamkufurisha ndugu yake Muislamu kwa dhana, na hii ni kutokana na kuwepo mgawanyiko ndani yake... Imekuja katika Kurrasah, ukurasa wa 12 word file: [...kuharamishwa kuitakidi kwa dhanni haimaanishi kukataa yale yaliyomo katika Hadith hizi na kutosadikisha yaliyokuja ndani yake, bali maana yake pekee ni kutoyachukulia kwa mkato (Jazm) yale yaliyomo ndani ya Hadith hizi, lakini yanakubaliwa na kusadikiwa, na yaliyoelezwa ndani yake yanasadikiwa kwa usadikishaji usiokuwa wa mkato. Kilichoharamishwa ni kuitakidi kwayo yaani kwa mkato (Jazm). Bali miongoni mwazo yamekuja maandiko yanayoagiza utendakazi hivyo basi yanatendewa kazi. Kutoka kwa Abu Hurayra amesema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «إِذَا فَرَغَ أَحَدُكُمْ مِنَ التَّشَهُّدِ الأَخِيرِ فَلْيَتَعَوَّذْ بِاللَّهِ مِنْ أَرْبَع، مِنْ عَذَابِ جَهَنَّمَ، وَمِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ، وَمِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ، وَمِنْ فِتْنَةِ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ » “Pindi anapomaliza mmoja wenu Tashahhud ya mwisho, basi naajilinde kwa Mwenyezi Mungu na mambo manne: kutokana na adhabu ya Jahannam, kutokana na adhabu ya kaburi, kutokana na fitina za uhai na mauti, na kutokana na fitina za Masih al-Dajjal” Imepokewa na Ibn Majah. عن عائشة أن النبي ﷺ كان يدعو في الصلاة: «اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَفِتْنَةِ الْمَمَاتِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ الْمَأْثَمِ وَالْمَغْرَمِ» “Na kutoka kwa Aisha kwamba Mtume (saw) alikuwa akiomba dua hii katika swala: “Ewe Mola hakika mimi najilinda kwako na adhabu ya kaburi, na najilinda kwako na fitina za Masih al-Dajjal, na najilinda kwako na fitina na uhai na mauti, ewe Mola hakika mimi najilinda kwako kutokana na madhambi na madeni” imepokewa na Bukhari. Hadith hizi mbili ni khabar ahaad, na ndani yake kuna maombi (talab) ya kitendo, yaani ombi la kuomba dua hii baada ya kumaliza Tashahhud, kwa hivyo ni imependekezwa (Mandub) kuomba kwa dua hii baada ya kumaliza Tashahhud, na yaliyoelezwa ndani yake yanasadikishwa na yanafanyiwa kazi, lakini hayawi ndani ya Aqida maadamu yamekuja katika Hadith ahaad, yaani kwa dalili dhanni, lakini yakija kwa njia ya upokezi wa wingi (Tawatur), basi hapo ni wajib kuyaitakidi...] Mwisho.
Nne: Sasa tunakuja kwenye Hadith ya Jibril (as), iliyotajwa katika swali hili, nayo ni Hadith iliyopokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abu Hurairah na ikapokewa na Muslim na wengineo kutoka kwa Abu Huraira na kutoka kwa Umar Ibn Al-Khattab, ambapo Jibril anamuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuhusu Uislamu, na akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «الْإِسْلَامُ أَنْ تَشْهَدَ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّداً رَسُولُ اللَّهِ ﷺ وَتُقِيمَ الصَّلَاةَ وَتُؤْتِيَ الزَّكَاةَ وَتَصُومَ رَمَضَانَ وَتَحُجَّ الْبَيْتَ إِنْ اسْتَطَعْتَ إِلَيْهِ سَبِيلاً» قَالَ: صَدَقْتَ، قَالَ: فَعَجِبْنَا لَهُ يَسْأَلُهُ وَيُصَدِّقُهُ! “Uislamu ni kushuhudia hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad (saw) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, na kufunga Ramadhan, na kuhiji Makkah kwa mwenye uwezo” akasema (Jibril): umesema kweli, akasema (Umar): tukamstaajabia, anamuuliza na huku anamsadikisha” قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنْ الْإِيمَانِ قَالَ: «أَنْ تُؤْمِنَ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ» قَالَ: صَدَقْتَ... قَالَ: ثُمَّ انْطَلَقَ فَلَبِثْتُ مَلِيّاً ثُمَّ قَالَ لِي: «يَا عُمَرُ أَتَدْرِي مَنِ السَّائِلُ» قُلْتُ: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: «فَإِنَّهُ جِبْرِيلُ أَتَاكُمْ يُعَلِّمُكُمْ دِينَكُمْ». Akasema (Jibril): nipe habari kuhusu Iman: akasema (Mtume): “Ni kumwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini Qadar kheri yake na shari yake inatoka kwa Mwenyezi Mungu.” Akasema (Jibril): ‘umesema kweli’... kisha akaondoka. Kwa hivyo nikasubiri kwa muda, kisha akaniambia (Mtume): “Ewe Umar je, unamjua muulizaji” nikasema (Umar): ‘Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajua zaidi’. Akasema (Mtume): “Hakika ni Jibril amewajieni kuwafundisha Dini yenu”
Hii ni Hadith sahih ambayo haijuzu kukataliwa, na wala haipingani na andiko la kukatikiwa, lakini haitoshelezi kipeke yake kuwa dalili katika Aqida... Hata hivyo, jumla ya mambo ya Aqida yaliyomo ndani yake yamekuja katika dalili nyenginezo za kukatikiwa (qat’i). Kwa hivyo nguzo za imani zimetajwa na aya tukufu za Qur'an, na pia nguzo za Uislamu... Hivyo basi, yote yaliyotajwa katika Hadith hii ni mambo ambayo yamebainishwa kwa dalili nyenginezo za kukatikiwa zisizokuwa Hadith hii, hivyo yanachukuliwa katika Aqida kwa dalili zake za kukatikiwa, kama vile kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):
﴾يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنْزَلَ مِنْ قَبْلُ وَمَنْ يَكْفُرْ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالاً بَعِيداً﴿
“Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali.” [An-Nisaa: 136] na akasema Mwenyezi Mungu (swt):
﴾آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنْزِلَ إِلَيْهِ مِنْ رَبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِنْ رُسُلِهِ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ﴿
“Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet'ii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.” [Al-Baqara: 285]
Vivyo hivyo, kuamini Qadar kwa maana ya elimu ya Mwenyezi Mungu na kuandikwa katika Ubao Uliohifadhiwa (Al-Lawh al-Mahfudh). Amesema Mwenyezi Mungu (swt): ﴿وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ قَدَراً مَقْدُوراً﴾ [Al-Ahzab:…] ﴿قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْراً﴾ [At-Talaq:…] ﴿مَا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِنْ شَيْءٍ﴾. ﴿كَانَ ذَلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُوراً﴾ [Al-Isra:...]. Hakuna kinachotokea isipokuwa kwamba kilikwisha kadiriwa na Mwenyezi Mungu, na kimeandikwa ndani ya Kitabu, yaani isipokuwa kimetanguliwa na elimu ya Mwenyezi Mungu, hivyo Qadar ni kinaya kwa elimu ya Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Kitabu ni kinaya kwa elimu ya Mwenyezi Mungu. Na kwa hiyo, Qadar katika Sharia maana yake ni kile kilichotanguliwa na elimu ya Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo maana yake kama ilivyoelezwa katika maandiko ya Qur’an na maandiko ya Sunnah.
Na vilevile nguzo za Uislamu ziko katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu:
﴾فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنْبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُم﴿
“Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa.” [Muhammad: 19]
﴾مُحَمَّدٌ رَسُولُ اللَّهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ تَرَاهُمْ رُكَّعاً سُجَّداً يَبْتَغُونَ فَضْلاً مِنَ اللَّهِ وَرِضْوَاناً﴿
“Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu.” [Fat’hi: 29]
﴾يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ﴿
“Enyi mlio amini! Mmefaradhishiwa Saumu, kama ilivyo faradhishwa kwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.” [Al-Baqara: 183]
﴾وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ﴿
“Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanao inama.” [Al-Baqara: 43]
﴾وَلِلَّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً﴿
“Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea.” [Aal-i-Imran: 97]
Hivyo basi Hadith hii haikataliwi bali hufahamiwa kwa sura yake kama ilivyo bainishwa hapo juu
Nataraji kwamba sasa imekuwa wazi.
Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
11 Jumada al-Awwal 1444 H
05/12/2022 M
Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa Facebook