- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Ujerumani na Mkakati wa Usalama wa Kitaifa
(Imetafsiriwa)
Swali:
Mnamo tarehe 14/6/2023, kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Ujerumani iliidhinisha mkakati wa kitaifa wa usalama wa taifa, baada ya mazungumzo yaliyochukua zaidi ya mwaka mmoja kati ya vyombo mbalimbali vya Ujerumani. Je, mkakati huu unawakilisha kumalizika kwa vikwazo vilivyowekwa kwa Ujerumani tangu kushindwa kwake katika Vita vya Pili vya Dunia mwaka wa 1945? Je, nini kinatarajiwa kwa Ujerumani baada ya kupitisha mkakati huu katika siasa za Ulaya na za kimataifa?
Jibu:
Ujerumani, kama nchi iliyoshindwa katika Vita Kuu vya Pili vya Dunia, iligawanywa katika sekta nne, kila moja ya nchi kuu zilizoshinda katika vita hivyo (Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza na Ufaransa) ikidhibiti sekta ndani yake, kisha nchi tatu za magharibi zikaanzisha Ujerumani Magharibi na Urusi ilianzisha Ujerumani Mashariki. Kivitendo Ujerumani Magharibi ilifuata Marekani kama dola tegemezi. Vile vile, Ujerumani Mashariki ilikuwa pamoja na Umoja wa Kisovieti (Urusi). Ujerumani Mashariki iliwakilisha kambi ya hali ya juu ya kijeshi kwa Umoja wa Kisovieti upande wa magharibi, na vilevile kwa Ujerumani Magharibi kwa Marekani kama kiongozi wa kambi ya magharibi kwa mashariki. Hii ilikuwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia… lakini uhalisia huu polepole ulibadilika baada ya hapo:
1- Isipokuwa baadhi ya mambo rasmi, serikali zote mbili za Ujerumani hakuna iliyokuwa na sera isiyotegemea kiongozi wa kambi, na hii iliendelea kuwa hivyo hadi Umoja wa Kisovieti ulipodhoofika na kukubali kuunganishwa kwa Ujerumani mwaka 1990, yaani, Moscow iliachana na Ujerumani Mashariki kwa upendelea wa upande wa Magharibi. Kwa kutiwa saini Mkataba wa Maastricht wa Umoja wa Ulaya mwaka 1992 licha ya Marekani na Urusi kuregeleaa matatizo yao ya ndani baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, Ujerumani imeanza kuibuka kuwa dola yenye nguvu kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya. Wajerumani waliona kwamba hali ya kimataifa imebadilika na kwamba kulikuwa na fursa ya kuweka kipengee cha uchumi kuwa nguzo ya msingi ya uhuru wa Ujerumani, hivyo Ujerumani ikaibuka kuwa yenye nguvu ya kiuchumi ikishindana na dola nyengine za Ulaya bila kuzichokoza dola nyenginezo za Ulaya; Uingereza na Ufaransa, au Kimataifa; Urusi na Marekani, haswa kwa kuwa sera ya ulinzi ya Ujerumani inajifunga na kiwango cha chini cha kijeshi.
2- Kwa mafanikio yake ya kiviwanda na kiuchumi na kupanuka kwa mahusiano yake ya kibiashara na Urusi, Ujerumani ilifanikiwa kuziongoza nchi za Ulaya kiuchumi, na uongozi huu wa Ujerumani uliwekwa kivitendo, kama ilivyokuwa katika mgogoro wa Ugiriki mwaka 2010. Kwa ujumla, mgogoro mkubwa wa kiuchumi ni jambo ambalo haliwezi kuhitimishwa barani Ulaya au katika uhusiano wa nje nayo bila Ujerumani. Ingawa hii haikuwa chanya kwa Ufaransa haswa, udhaifu wa jeshi la Ujerumani ulikuwa ukipendekeza kwa Ufaransa kila wakati kwamba mashindano kati ya nchi hizo mbili bado yalikuwa ndani ya mfumo wake mzuri wa michezo. Katika vipindi hivyo, Ujerumani ilikuwa ikitoa dira yake ya changamoto za kiusalama kupitia vitabu vya kizungu vilivyotolewa na Wizara yake ya Ulinzi, cha kwanza kilikuwa mwaka 1969 na cha mwisho 2016, na kilikuwa kinazungumzia usalama na ugaidi na kutaka kushiriki, lakini kupitia Umoja wa Mataifa, na wakati Urusi mwaka 2014 ilipoivua Crimea kutoka Ukraine na kuiunganishe kwake, Ujerumani ilipinga vikali jambo hilo na kushiriki katika vikwazo vya Magharibi dhidi ya Urusi, lakini maslahi yake ya kibiashara yaliyokua pamoja na Urusi yalikuwa yakiizuia Urusi kutoongoza hatua zozote dhidi ya Urusi. Licha ya mazungumzo kwamba Urusi inaharibu mizani ya usalama ya Ulaya kwa kuinyakua Crimea, ushiriki wa Ujerumani katika makubaliano ya Minsk ulileta matumaini kwa Wajerumani kusitisha vitisho vya Urusi kwenye mipaka ya Crimea na Donbass, ambapo Urusi ilianzisha vita mwaka huo na kuwaunga mkono waasi wa Urusi dhidi ya serikali ya Ukraine.
3- Lakini kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022 na ukinaifu wa Marekani kwamba Urusi inaharibu tu misingi ya usalama wa kimataifa iliyojengwa na Marekani, dhurufu za Ulaya na kimataifa zimeungana ili kuipa Ujerumani fursa ya dhahabu ya kujenga nguzo nyingine ya kijeshi pamoja na nguzo imara ya kiuchumi ndani yake. Hiyo ni kwa sababu Marekani inazitaka dola za Ulaya zisimame kwa niaba yake, kukabiliana na Urusi ili Marekani ijiandae na iwe tayari kusitisha kuinuka kwa China. Hapa Ujerumani iliona kuwa uwanja wa kimataifa umekuwa wazi kwa Ujerumani kuibuka kuwa nchi yenye nguvu kubwa ya kijeshi, na kwa kukata uhusiano wake wa kibiashara na Urusi, Ujerumani ilitangaza kuanzisha mfuko mkubwa wa kifedha wenye thamani ya euro bilioni 100 kusaidia jeshi lake na maendeleo yake ili kuweza kudumisha usalama wake. Ilitangaza kwamba vita vya Ukraine viliwakilisha hatua ya mabadiliko, na hata kupeleka ndege zake za kivita mbali sana kwenye Bahari ya Pasifiki katika ishara kali kwamba jeshi la Ujerumani lilikuwa limeanza kukwepa vikwazo baada ya Vita vya vya pili vya Dunia, na hivyo hisia za ukuu zilisisimka kwa watu wa Ujerumani. Ujerumani ilizungumza kuhusu ahadi zake maalum kuelekea Ukraine na hata kuelekea Ulaya Mashariki, na kulikuwa na mazungumzo mengi nchini Ujerumani kuhusu haja ya kuwa tayari kukabiliana na tamaa za kibeberu za Urusi ambazo hazitaishia kwenye mipaka ya Ukraine.
4- Serikali ya Chansela Scholz, wakati wa uwasilishaji wake wa mkakati wa usalama wa taifa 14/6/2023, ilikuwa na nia ya kuonyesha makubaliano ya Wajerumani kuhusu mkakati huu. Wawakilishi wa vyama vya Ujerumani katika muungano wa serikali walikuwepo na Chansela wakati wa uwasilishaji wake, nao ni mawaziri wa chama cha Green Party na Free Democratic Party pamoja na chama cha Chansela Scholz (Socialist Democrat). Hii inaashiria uzito wa mabadiliko haya ndani ya Ujerumani na athari zake katika kuihamisha Ujerumani kutoka katika nafasi ya kijeshi na kiusalama ambayo iliendelea nayo kwa miongo kadhaa baada ya Vita vya Pili vya Dunia hadi eneo jipya, ingawa vyama vya upinzani vimetoa tuhma nyingi dhidi ya serikali za upofu fulani katika mkakati huu.
5- Labda taarifa ya Chansela wa Ujerumani Scholz inaelezea mabadiliko mapya ya ubora huu katika sera ya Ujerumani:
[Chansela wa Ujerumani alisisitiza kuwa Mkakati wa Usalama wa Kitaifa ulioidhinishwa na serikali ya Ujerumani leo ni mchango muhimu katika kuhakikisha usalama wa watu nchini Ujerumani kwa kuzingatia mabadiliko ya mazingira. Mwanasiasa huyo wa Kijerumani wa chama cha Social Democrat alisema kuwa Baraza la Mawaziri la Ujerumani, katika kuidhinisha mkakati huu, lilifanya uamuzi usio wa kawaida na muhimu. Scholz alieleza kuwa mazingira ya usalama-kisiasa ya Ujerumani yamebadilika sana kwa kuzingatia shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine na kuonekana kwa uchokozi zaidi wa serikali ya China. Scholz alisema kuwa jukumu kuu la serikali ni kufanya kazi ili kuhakikisha usalama kwa raia bila makubaliano yoyote, akionyesha kuwa kazi hii itafanywa kupitia mkakati wa usalama unaofuata kanuni elekezi ya usalama jumuishi. Aliendelea kuwa kile kilichokuwa na kikomo katika upangaji wa serikali ya Ujerumani huko nyuma kwa sera ya ulinzi pekee, sasa kitafuata mtazamo kamili na wa kina (Deutsche Welle, Ujerumani, 14/6/2023)].
6- Waraka wa mkakati wa usalama wa taifa wa Ujerumani unawakilisha kanuni zinazoongoza serikali ya Ujerumani kudumisha usalama wa watu wake. Moja ya kanuni muhimu iliyopitishwa tangu Vita vya pili vya Dunia, ambayo ilitupiliwa mbali katika waraka huu, ni kwamba jeshi la Ujerumani linafanya kazi za ulinzi kushughulikia vitisho vya usalama na kuhamia kutekeleza vitendo vya kina, ambavyo ni pamoja na kushambuli. Haya ni maendeleo hatari sana katika Ulaya. Waraka huo unataja maendeleo ya kina na ya haraka ya jeshi la Ujerumani. Mbali na kusisitiza kujitolea kwa uamuzi wa NATO wa mwaka 2014 wa kutumia angalau asilimia 2 ya pato la taifa kwa manufaa ya jeshi na usalama. Ujerumani inaziandaa wizara nyenginezo kupunguza bajeti zao kwa ajili ya jeshi. Haya pia ni mabadiliko makubwa katika kupunguza mtazamo wa ustawi wa Wajerumani. Waziri wa Fedha Christian Lindner alisema: [Ujerumani kwa miongo mingi "iliishi kwa faida ya amani". Hii ina maana kwamba iliaminika kwamba hakukuwa na haja ya kuzingatia sana suala la ulinzi. "Hii ina maana kwamba hisa katika bajeti zitaleta mabadiliko ya kudumu," alisema Waziri wa Fedha jijini Berlin wakati akiwasilisha mkakati huo. (Deutsche Welle, Ujerumani, 16/6/2023)].
7- Waraka huo pia unawakilisha mtazamo wa serikali ya Ujerumani juu ya uchambuzi wa hatari, kwani jeshi la Urusi linasimama mbele ya hatari za nje, au kile walichokiita shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine, na baada ya hapo, yaani, kwa kiwango kidogo, kusimama dhidi ya hatari kuinuka kwa China na utawala wake, ambao wanauita huko Magharibi kuwa wa kimabavu, kama ilivyoelezwa katika taarifa za Scholz (kuibuka kwa ari ya serikali ya China). Waraka huo hauangalii hatari za ndani kama vile usalama wa mtandaoni na uzito wa tishio hilo kwa miundombinu ya Ujerumani na mabadiliko ya tabianchi, ingawa masuala haya yanahusiana moja kwa moja na tishio kutoka nje ya nchi, kwani Urusi inatuhumiwa kufanya mashambulizi ya mtandaoni katika nchi za Magharibi. Pamoja na uratibu wa kimataifa ili kupunguza hatari za mabadiliko ya tabianchi, ikimaanisha kuwa mkakati huu wa Ujerumani kwa usalama wa taifa unawakilisha mabadiliko ya Ujerumani kutoka hali moja hadi nyingine katika sera yake ya nje, ingawa baadhi ya shaka na tashwishi bado zinatawala fikra za kisiasa nchini Ujerumani.
8- Kwa kuimarisha jeshi lake na kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya maendeleo yake na kufungua njia kwa ajili ya vitendo vya kijeshi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi, Ujerumani itakuwa imeondokana na eneo la kijeshi ililowekwa juu yake katika kile kinachojulikana kama vikwazo vya baada ya Vita vya pili vya Dunia, ikimaanisha kuwa utata huu umekuwa historia. Hili linazua tofauti kubwa na za kimsingi. Baina yake na Ufaransa, tofauti hizo zinaonekana waziwazi leo, ingawa Ujerumani, ambayo ilitia saini Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia, bado inajitolea kwa hali yake isiyo ya nyuklia, ambayo ilithibitishwa mnamo 1990 katika "Mkataba wa Suluhisho la Mwisho kuhusiana na Ujerumani" iliyotiwa saini na dola kubwa nne baada ya kuungana kwake mwaka huo huo. Ili kuelewa undani wa mabadiliko haya nchini Ujerumani, kuimarishwa kwa jeshi la Ujerumani kunahitaji kuongezeka kwa idadi yake, na hii inagongana na ahadi za Ujerumani katika "Mkataba wa Suluhisho la Mwisho kuhusiana na Ujerumani" uliotiwa saini na dola kubwa mnamo 1990 ili kuiunganisha Ujerumani, mkataba ambao uliweka kiwango cha juu kwa jeshi la Ujerumani na idadi ya juu ya wanajeshi elfu 370, lakini Marekani, pamoja na Uingereza, ziliisukuma Ujerumani kucheza dori mpya katika kukabiliana na Urusi, ambayo itawezesha Ujerumani kukataa makubaliano haya, na hii itawakilisha kuondoka kwa Ujerumani kutoka kwa vikwazo vyovyote vya Urusi kwa nguvu zake za kijeshi. Ama Ufaransa, msimamo wake unaonekana kuwa dhaifu mbele ya mielekeo ya Marekani na Uingereza ya kuiimarisha Ujerumani. Hakika, mzozo unaokua wa Ujerumani na Ufaransa unaweza kufanya kazi kudhoofisha Muungano wa Ulaya kwa jumla, ambao unakaribishwa na Marekani na Uingereza.
9- Ili kupunguza hofu ya Wafaransa, hasa ya kuongezeka kwa jeshi la Ujerumani, mkakati wa Ujerumani unazungumzia Ujerumani kama sehemu ya Muungano wa Ulaya: [Serikali iliweka katika mkakati huo mkusanyiko wa malengo, kama vile ulazima wa kuimarisha teknolojia ya ulinzi katika ngazi ya Ulaya, na kuimarisha makabiliano ya ujasusi, hujuma na mashambulizi ya mtandao. Mbali na ulazima wa kuratibu udhibiti wa usafirishaji wa Silaha katika ngazi ya Muungano wa Ulaya (Deutsche Welle, 16/6/2023)]. Hata hivyo, kwa upande mwingine, kuna hofu ya aina nyingine jijini Paris, ambayo inaona kwamba mikakati ya Ulaya imekuja kutolewa kutoka Berlin, kwani Ujerumani pia inaongoza mradi wa Ulaya wa ulinzi wa anga. [Mkakati huo mpya unaitaja Ujerumani kuwa ndio nchi kubwa zaidi barani Ulaya katika suala la idadi ya watu na uwezo wa kiuchumi, na hivyo kwa kile kinachohitajika ili kuimarisha mfumo wa ulinzi wa Ulaya na NATO. Inaashiria hamu ya Ujerumani kucheza dori kuu hapa, haswa inapotafuta kujenga ngao ya anga ya makombora ya Ulaya ya Sky Shield. Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius alitangaza kwamba nchi 18 zimeelezea makubaliano yao kimsingi kushiriki katika mpango huu (Al-Sharq, 17/6/2023)].
10- Kuhusiana na mtazamo wa China na Urusi kama tawala za kimabavu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Baerbock anasema katika maelezo yake kuhusu mkakati wa usalama wa taifa: [Mkakati huo umejikita katika "vipimo vitatu kuu" vya sera ya usalama: ulinzi, uthabiti na uendelevu. Sehemu ya ulinzi ni pamoja na kuimarisha jeshi, ulinzi wa raia na kulinda raia. Katika uwanja wa Ustahimilivu, yaani, uwezo wa kuzuia, unahusu kuhami "mfumo wetu wa msingi wa kidemokrasia dhidi ya ushawishi haramu wa nje" pamoja na kwamba "matokeo ya upande mmoja katika uwanja wa malighafi na usambazaji wa nishati" yanapaswa kupunguzwa na vyanzo vya usambazaji kuongezwa (Deutsche Welle, 16/6/2023)]. Na katika mabadiliko haya makubwa ya Ujerumani nyuma ya sera ya Marekani ya kupunguza silsila za usambazaji za China, baada ya Marekani kuilazimisha Ujerumani na Ulaya yote kukata silsila nyingi za usambazaji wa nishati kutoka Urusi. Jambo hili liko wazi na halina utata katika taarifa za Ujerumani, kulingana na Chansela Scholz, kulingana na chanzo kile kile cha awali, "Kwetu sisi, uhusiano na Muungano wa Ulaya na muungano wa nchi za kati ya Atlantiki unabaki kuwa mkuu."
11- Kwa hivyo, vipimo vya mkakati huu wa usalama wa kitaifa wa Ujerumani vinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:
a- Mkakati huu unakomesha uimara wa jeshi la Ujerumani uliolazimishwa juu yake tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, huku Ujerumani ikiendelea kwa kasi kuelekea kuimarisha jeshi lake na kulifanya kuwa mdhamini wa usalama wake, lakini Ujerumani inavunja vikwazo kadri dhurufu za kimataifa zinavyoruhusu, kwani imesalia kuwa mtiaji saini mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia.
b- Kwa mujibu wa masharti ya kimataifa ya Magharibi, Ujerumani inawafafanua maadui zake ipasavyo kuwa ni jeshi la Urusi katika nafasi ya kwanza, na katika nafasi ya pili China. Ni mkakati gani wa Ujerumani unazungumzia kuwa mshirika wa kibiashara na nchi yenye mtazamo mkali kuelekea mazingira yake, lakini haubatilishi ushirikiano nayo katika kutatua matatizo ya kimataifa. Msimamo wake kuelekea hilo unafanana kabisa na msimamo uliotajwa wa Kundi la Saba.
c- Ujerumani inafafanua changamoto za usalama na kijeshi zinazoizunguka kama nchi mwanachama wa Muungano wa Ulaya na mwanachama wa NATO. Mkakati wa Ujerumani unathibitisha kujitolea kwa Ujerumani kufanya kazi kupitia vyombo hivi vya Ulaya na kimataifa.
d- Iwapo mkakati huu utathibitisha kwamba Ujerumani ni sehemu ya Ulaya na sehemu ya nchi za NATO na inazungumzia usalama wake kama sehemu ya usalama wa pamoja wa mfumo wa Ulaya na mfumo wa Atlantiki na kuthibitisha kwamba inatetea mfumo wa kimataifa ambao Marekani inaudhibiti, hii haipunguzi hatari ya mkakati huu wa Ujerumani. Wala haipuuzi ukweli kwamba mkakati huu wa Ujerumani unawakilisha moja ya hasara kubwa ya kimataifa kwa Moscow, kama vile Sweden na Finland kujiunga na NATO.
e- Na ikiwa Ujerumani imetumia katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita nafasi yake ndani ya Muungano wa Ulaya kuangazia uongozi wake katika masuala ya kiuchumi, basi ilikuwa ni hatua yake ya kwanza kuelekea ukuu, na sasa inachukua fursa ya vita vya Ukraine na dhurufu za kimataifa zinazoizunguka kuunda jeshi imara na kambi ya viwanda ya kijeshi kama hatua yake ya pili kuelekea ukuu. Hii inaiwezesha kujinasua kutoka kwa vikwazo vyengine na kujenga mkakati wa Ujerumani tofauti na nchi za Ulaya na kujitenga na Marekani, na ingawa hii haitarajiwi kwa muda mfupi, matukio yanaonyesha kwamba Ujerumani itafuata njia hii.
12- Kwa kumalizia, dola kubwa duniani leo zinashindana wao kwa wao kumwaga damu kwa dhulma na ufasiki, kwa kueneza ufisadi katika ardhi, na kuangamiza mazao na vizazi. Hali ya watu haitaboreka isipokuwa ardhi ing’arishwe tena kwa nuru ya Khilafah, na kuregesha usalama na amani sio tu kwa Waislamu pekee, bali kwa yeyote yule ambaye kivuli chake kitamfikia na kisha haki isikike katika pembe zote za dunia.
[وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقاً]
“Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!” [Al-Isra’: 81]
[وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيباً]
“na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu!” [Al-Isra’: 51]
5 Dhul Hijjah 1444 H
23/6/2023 M