Jumatatu, 08 Dhu al-Hijjah 1447 | 2026/05/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Wilayah Afghanistan

H.  5 Dhu al-Hijjah 1447 Na: Afg. 1447 H / 11
M.  Ijumaa, 22 Mei 2026

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Umaskini Ulioenea na wa Kimuundo Nchini Afghanistan: Matokeo ya Kufeli Kutabikisha Mfumo wa Kiuchumi wa Uislamu—Na Uendelevu wa Fikra ya Kiuchumi ya Enzi ya Jamhuri

(Imetafsiriwa)

Ripoti za hivi karibuni—ikiwa ni pamoja na ripoti ya kushtua ya BBC kutoka mkoa wa Ghor, kujichoma moto kwa mhandisi jijini Kabul, na simulizi zinazorudiwa rudiwa za watu wanaouza figo—zimefichua janga la kibinadamu linaloumiza moyo wa kila Muislamu. Katika baadhi ya miji, foleni ndefu za watu wanaotafuta kazi, njaa, na umaskini zimekuwa uhalisia unaoonekana. Wengine, wakiwa wamekandamizwa na umaskini na madeni, wamelazimika kuwauza binti zao wadogo ili kuokoa maisha ya wanafamilia wengine. Ripoti za UNDP zinaonyesha kwamba watu watatu kati ya kila wanne nchini Afghanistan hawawezi kukidhi mahitaji yao ya msingi ya maisha, na zaidi ya asilimia kumi ya idadi ya watu wako ukingoni mwa njaa.

Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir / Wilayah Afghanistan inasisitiza kwamba mizizi ya mgogoro huu haiko tu katika ukame au kusitishwa kwa misaada ya kigeni, bali katika miundo ya kiuchumi isiyo salama na mwendelezo wa fikra ya kiuchumi ya enzi ya jamhuri na sera za uchumi zinazoegemea juu ya msingi wa ubepari. Maafisa wa sasa wanaelezea umaskini uliopo kama matokeo ya kuanguka kwa “uchumi bandia” wa miaka ishirini iliyopita; lakini hoja hii haifichi uhalisia mchungu wa kutokuwepo kwa usambazaji adilifu wa utajiri.

Afghanistan si nchi maskini kwa upande wa rasilimali. Ardhi hii ina akiba kubwa ya madini, ardhi ya kilimo, maji, nafasi muhimu ya kijiografia, nguvu kazi changa, na uwezo mkubwa wa uzalishaji. Tatizo kuu si ukosefu wa rasilimali, bali ni ukosefu wa mfumo unaosimamia rasilimali hizi kwa msingi wa uadilifu, uwazi, na uwajibikaji unaotegemea Sharia.

Leo, rasilimali za kiuchumi, nyadhifa za utawala, na fursa za kazi kwa kiasi kikubwa hufanyiwa ukiritimba na duara chache na washirika wa watawala, huku uchimbaji wa madini—unaofanywa bila uwazi au ushindani adilifu—umejilimbikizia utajiri mikononi mwa makundi maalum. Hii ndiyo mantiki halisi ya mfumo wa kibepari: badala ya kupata mahitaji muhimu ya watu, inazingatia ukuaji wa juujuu wa uchumi na “soko”—soko linalolimbikiza utajiri mikononi mwa wachache na kuwasukuma walio wengi katika maangamivu.

Hoja yetu, inayotegemea msingi wa Uislamu, iko wazi:

Katika Uislamu, umaskini ni hali ya mtu binafsi kutoweza kupata mahitaji ya msingi—kama vile chakula, mavazi, na makaazi. Kutoweza kwa mfumo kutoa mahitaji haya kunamaanisha sera zake za kiuchumi zimefeli.

Tatizo la kiuchumi si ukosefu wa rasilimali, bali ni usambazaji usio adilifu wa utajiri. Uchumi uliofanikiwa haupimwi kwa kiasi cha uzalishaji au ongezeko la mapato ya serikali; badala yake, mafanikio yake halisi hupimwa kwa uwezo wake wa kusambaza utajiri na kupata mahitaji ya msingi ya kila mtu. Uislamu unailazimisha serikali kuhakikisha kwamba utajiri unamfikia kila mtu, ilhali serikali ya sasa imefeli kujenga uchumi wenye natija pamoja na kusambaza utajiri kwa uadilifu.

Katika mfumo wa Kiislamu, ikiwa mtu hawezi kufanya kazi, au ikiwa hakuna fursa ya kufanya kazi inayopatikana, kukidhi mahitaji ya mtu huyo kwanza ni jukumu la jamaa wa karibu na kisha jukumu la Bayt al-Mal (hazina ya umma), kwamba baba alazimishwe kumuuza mtoto wake mwenyewe ili tu kulipia matibabu ya mtoto au kununua chakula ni ushahidi wa kuporomoka kwa jukumu kwa upande wa serikali na jamii.

Migodi mikubwa ya dhahabu, mafuta, na gesi ni “mali ya umma”, na mapato yake lazima yatumike kwa ustawi wa watu—yasiwekwe mikononi mwa makampuni binafsi, dola za kivita, au duara maalum za utawala. Mbinu ya sasa, kwa kweli, si kitu chengine ila uporaji uliopangwa wa utajiri wa Ummah.

Watawala wa sasa wa Afghanistan lazima waelewe kwamba njia za kuzuia kivitendo, kutoza kodi kubwa kwa watu maskini, na kuweka matumaini kwenye miradi na misaada kutoka kwa dola za kikoloni haziwezi kujaza matumbo matupu ya maskini na yatima. Njia ya wokovu ni kuachana kikamilifu na mabaki ya fikra ya kiuchumi ya jamhuri na sera za uchumi wa kibepari, na kurudi kwenye mfumo wa kiuchumi wa Uislamu chini ya Khilafah Rashida—mfumo ilioasisiwa juu ya uadilifu, utu wa binadamu, na usambazaji mzuri wa utajiri, ambao hauchukulii umaskini kama hali ya kimaumbile bali kama hali maalum ambayo lazima iondolewe.

[وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا]

“Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki.” [Ta-Ha: 124]

Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Afghanistan

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Wilayah Afghanistan
Address & Website
Tel: 
http://hizb-afghanistan.org/
E-Mail: info@hizb-afghanistan.org

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu