Afisi ya Habari
Afrika Mashariki
H. 5 Jumada II 1437 | Na: 1437/08 H |
M. Jumatatu, 14 Machi 2016 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Haifanyi Kazi Kuipindua Serikali ya Kenya
Mashirika ya habari yameripoti kesi inayomkabili Arkanuddin Yassin mwanaharakati wa Hizb ut Tahrir ambaye alifikishwa katika Mahakama ya Milimani Nairobi mnamo Jumatano 9 Machi 2016; kwa mashtaka ya kubeba fikra za Khilafah ambazo kwazo anataka kuipindua Serikali ya Kenya. NTV ilimtaja Arkan kama "Mhubiri wa Chuki".
Kwa kuwa fikra za Khilafah ni za Kiislamu na zinalinganiwa na Chama cha Kisiasa cha Kiislamu cha Kimataifa Hizb ut Tahrir; hivyo basi tungependa kufafanua yafuatayo:
Hizb ut Tahrir iliasisiwa mnamo 1953 kama Chama cha Kisiasa cha Kiislamu kinacholenga kusimamisha tena Uislamu kama Dola katika ulimwengu wa Waislamu. Hizb ut Tahrir kamwe haijawahi na haitawahi kutumia ghasia au vitendo vya kijeshi kama njia yake ya kusimamisha tena Khilafah kwa njia ya Utume
Khilafah ilikuwa ndio utawala mkuu wa Uislamu uliotawala nusu ya ulimwengu ikiwemo baadhi ya maeneo ya Afrika. Kwa kipindi cha karne 13, Khilafah ili dhamini utulivu, amani na usalama kwa watu wote Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Kama ambavyo Uislamu umewafaradhisha vitendo vya ibada kama Hijab, Swala na Saumu, vilevile umefaradhisha kitendo cha kusimamisha tena Khilafah. Hizb ut Tahrir inabeba msimamo wa Kiislamu kuwa baada ya Kuvunjwa Khilafah mnamo 1924 imekuwa ni faradhi kwa Waislamu duniani kuyarudisha maisha kamili ya Kiislamu kupitia kusimamisha tena Khilafah katika biladi za Waislamu. Hizb ut Tahrir inabeba jukumu la ulinganizi huu kote katika ulimwengu wa Waislamu ikiwemo Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla.
Kazi ya Hizb ut Tahrir katika mataifa kama Kenya ni kujenga Fahamu ya Kiislamu kwa Waislamu juu ya Uislamu ili wautafakari na wawe na Utambulisho wa kweli wa Kiislamu. Hizb ut Tahrir haifanyikazi kusimamisha tena Khilafah nchini Kenya wala kuipindua serikali ya Kenya kwa sababu Kenya haina vipimo vya kisheria vya kuanza na kusimama tena Khilafah. Kwa zaidi ya miaka 20 sasa, Hizb ut Tahrir nchini Kenya kamwe haijahusika na vitendo vyovyote vya ghasia na mauaji ya aina yoyote ile.
Katika makongamano na warsha zake, Hizb ut Tahrir huwaalika wasomi kutoka katika nyanja zote za maisha na miongoni mwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu kushirikiana nao kwa jumla katika mazungumzo ya kifikra yanayoonyesha utukufu na uwezo wa Uislamu katika kutatua matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayoukumba ulimwengu leo. Hizb ut Tahrir inabeba Ulinganizi wa Kiislamu kupitia kuonyesha kuwa Uislamu ni muongozo mpana wa maisha ulio na suluhisho kwa matatizo yanayowakumba wanadamu. Vilevile, inaamini kuwa ulimwengu leo umo ndani ya majanga kwa sababu ya mfumo wa kikoloni wa Kimagharibi wa Urasilimali. Mfumo unaobebwa na Wamagharibi wanaofuja rasilimali za nchi changa ikiwemo Kenya. Hizb ut Tahrir haina uhusiano wowote na makundi yoyote yanayotumia vita kama njia ya kusimamisha tena Khilafah.
Ama kumuita Arkan 'Mhubiri wa Chuki', hili kwa hakika ni uchochezi wa chuki dhidi ya Uislamu na ulinganizi wake. Na tunajua kwamba mojawapo ya silaha zinazotumiwa na Wamagharibi kuuonyesha Uislamu kama mwangaza mbaya ni vyombo vya habari. Mara kwa mara vyombo vingi vikubwa vya habari havitoi jukwaa la haki na uadilifu la kulingania Uislamu; lakini badala yake vinaegemea katika propaganda chafu huku vikiwa havijali kusikiliza upande halisi na sahihi wa Uislamu. Na tunajua waziwazi kuwa vyombo vya habari aghalabu huweza kutumiwa kuitumbukiza nchi ndani ya vurugu ikiwemo Vita vya Kidini.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi wa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Afrika Mashariki
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Afrika Mashariki |
Address & Website Tel: +254 717 606 667 / +254 737 606 667 www.hizbuttahrir.today |
E-Mail: abuhusna84@yahoo.com |