Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Dola ya Kiislamu: Suluhisho kwa Ukandamizaji wa ‘Waliowachache’

(Imetafsiriwa)

Katika vyuo vikuu, wanafunzi wanashajiishwa kufuata fikra za kiliberali. Wanaambiwa kuwa hiyo ndio njia pekee ya wao kuwa ni wasiopendelea upande wowote na ‘kuwakubali’ wote walio wachache. Kwa sababu tusipokubali kuchukua fikra za kiliberali, tutakuwa na mapendeleo na kuwa dhulma. Fikra hizi zimekuwa zikivutia zaidi, kwani watu wamekuwa wakiangalia duniani kote na kuona jinsi jamii za wachache zinavyotendewa uovu. Wanaambiwa kuwa kama kuna udhalimu katika nchi zisizo za Wamagharibi, basi ni kwa sababu hazijawa katika kufuata uliberali vya kutosha. Na kama kuna udhalimu katika nchi za Magharibi, ni kwa sababu watu wachache ni waovu, lakini mfumo upo kwa kila mtu.

Hii sio sahihi.

Licha ya hizo hoja, kinyume chake ni kuwa haki za binaadamu ni zenye dosari. Kuna mvutano unaoendelea ndani ya jamii juu ya nani atatawala kwani kuwa katika nafasi ya utawala kunawapa nguvu za kufanya imani zao au tamaduni zao kuwa juu ya nyengine; wale wasio na nguvu, hawahakikishiwi haki zao za msingi za kibinaadamu.

Katika Uislamu, mambo ni tafauti. Dhana ya wachache haipo. Ima uwe ni raia wa Dola ya Kiislamu ama la. Na kuwa raia wa Dola ya Kiislamu humaanisha kuwa unapatiwa hifadhi ya mali na mwili vyote pamoja.

“Raia wote wa dola wanapaswa kuamiliwa kwa usawa bila kuzingatia dini, kabila, rangi au kitu chengine chochote. Dola hairuhusiwi kubagua baina ya raia ima iwe upande wa hukmu, au kuangalia mambo yao.” (Kifungu cha 6 cha Kielelezo cha Katiba)

Fauka ya hayo, "Kila raia aliyebaleghe na mwenye akili timamu ana haki ya kuwa mwanachama katika Baraza la Umma (Majlis al-Umma). Sawa sawa awe mwanamume au mwanamke, Muislamu au la. Isipokuwa uanachama wa asiyekuwa Muislamu umefungika katika kutoa sauti ya malalamiko kuhusu dhulma zinazofanywa na watawala wao au utabikishaji mbaya wa Uislamu juu yao." (Kifungu 103 cha Kielelezo cha Katiba)

Na Mtume (saw) amesema

«مَنْ ظَلَمَ مُعَاهِدًا أَوْ انْتَقَصَهُ أَوْ كَلَّفَهُ فَوْقَ طَاقَتِهِ أَوْ أَخَذَ مِنْهُ شَيْئًا بِغَيْرِ طِيبِ نَفْسٍ فَأَنَا حَجِيجُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ»

“Yeyote anayemdhulumu Mu’ahid (Kafiri aliye chini ya mkataba) au kumvunjia heshima au kumkalifisha zaidi ya uwezo wake au kuchukua kitu kwake bila kuridhia basi nitakuwa mpinzani wake siku ya kiyama” (Abu Dawuud). Pia Mtume (saw) amesema

«مَنْ قَتَلَ مُعَاهَدًا لَمْ يَرِحْ رَائِحَةَ الْجَنَّةِ وَإِنَّ رِيحَهَا تُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ أَرْبَعِينَ عَامًا»

“Yeyote anayemuuwa Mu’ahid hatoisikia harufu ya Pepo, na harufu yake inapatikana umbali wa mwendo wa miaka arubaini.” (Bukhari)

Kama tunavyoona kutokana na dalili, utafauti uliopo ni baina ya raia Muislamu na asiye Muislamu. Lakini hata hivyo, tafauti hiyo haihusiani na usimamizi wa mambo ya raia: kwani hairuhusiki kwa Dola kubagua au kutenganisha baina ya raia wake bali ni wajibu kwake kuwashughulikia wote kwa usawa bila kubagua kwa msingi wa kabila, rangi, jinsia au Dini.

Baadhi ya watu wanahoji kuwa kutafautisha baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu ni ubaguzi, kwa kuwa Waislamu wanapatiwa haki ambazo wengine hawapatiwi na hasa katika eneo la ushiriki wa kisiasa.

Ili kufahamu kuwa hivi sio hali ilivyo, tunapaswa kufahamu uhalisia wa sheria za Uislamu. Uislamu una mfumo ulio kamili katika mambo yake yote ya maisha. Japokuwa mfumo huu umetokana na Aqida ya Kiislamu, lakini haujajifunga tu kwa upande wa kiroho. Pia unawakilisha sheria na hukmu zenye uwezo wa kujitegemea katika kutumika ndani ya Dola. Wakati Uislamu ulipoamrisha utabikishaji wa mfumo huu, uliuangalia kutoka kwenye sheria na muono wa hukmu na sio kutoka kwenye mtazamo wa kidini. Umelazimisha utumiaji wa Hukmu za Sharia kwa raia wote wa Dola bila kuzingatia tafauti zao za Dini isipokuwa kwenye Hukmu ambazo ni maalum kwa watu wa Dini maalum na ambapo upande wa Dini umetawala.

Unawaangalia wanaadamu kwa mujibu wa uwanaadamu wao na imeufanya wito wake kuelekezwa kwa mwanaadamu. Sheria za Kiislamu zinazingatia matatizo yote ya mwanaadamu kuwa ni matatizo ya mwanaadamu pekee na sio ya kitu chengine chochote; tatizo linahitaji suluhisho, na suluhisho ni kwa kulingana na tatizo lenyewe. Kwa hiyo, sheria katika Uislamu haziruhusu ubaguzi katika Hukmu zake kabisa. Hii haimaanishi kuwa inatoa hukmu moja kwa watu wote kuhusiana na kila suala bali inazingatia sifa maalum katika sheria zake ambazo zinakisi uhalisia wa suala hilo ambalo linahitaji kutatuliwa. Kwa mfano wakati Uislamu unapanga na kusimamia mahusianao ya mwanamme na mwanamke, unazingatia sifa za mwanamume na mwanamke kutokana na mahusiano yao ya moja kwa moja yanayohusu suala hili. Vivyo hivyo, tunapoangalia tafauti baina ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu, inadhihirika kuwa tafauti hii imefanya kuwa ni hitajio kutokana na maumbile ya suala (Mas’alah) hili na kuwa hili ni muhimu; hata hivyo, huu sio ubaguzi.

Kwa mfano, Uislamu umefanya imani katika Uislamu kuwa ni sharti kwa Haakim (mtawala) na haujaruhusu nafasi hizi zishikiliwe na asiyekuwa Muislamu. Hii ni kwa sababu Dola ya Kiislamu inatekeleza Sheria za Kiislamu ndani ya Dola na kueneza ujumbe wa Uislamu duniani kwa njia ya Da’wah na Jihad. Kwa namna hiyo, dori na kazi ya Mtawala ndani ya Dola ya Kiislamu inazunguka katika utekelezaji wa Ahkam za Uislamu na kuchunga maslahi ya watu kwa mujibu wa Ahkam za Shariah pamoja na kubeba Ulinganizi wa Uislamu kwa wasiokuwa Waislam nje ya Dola. Matendo haya kutokana na maumbile yake yanahukumu na kumtaka yule anayeyatekeleza awe tayari ameuamini Uislamu kuwa ndio Aqida na Sheria kwani haiwezekani kuwa Uislamu utekelezwe na kutumika na kuwa Da’wah ienezwe duniani na yule ambaye hauamini.

Kuna Hukmu za Sharia nyingi ambazo zinawapa Ahlu dhimmah (raia wasio Waislamu wanaoishi ndani ya Dola ya Kiislamu) haki ambazo hazifikiwi na kupatiwa Waislamu; hata hivyo, hii haiwi ni aina yoyote ya ubaguzi au kupewa upendeleo Ahlu dhimmah dhidi ya Waislamu, bali ni kuzingatia namna hizo mbili, Uislamu na Ukafiri, na kuunganishwa kwao na suala maalum. Ndio hivyo hivyo Sharia imefanya zaka kuwa ni wajibu juu ya Waislamu wakati haikuifanya wajibu juu ya Ahlu dhimmah kwa sababu hii ni ibadah na haisihi ibadah kwa watu wa Dhimmi. Sharia pia imewajibisha Waislamu kulipa kodi katika wakati ambapo kuna haja kwa hilo, lakini haijawajibishwa hiyo juu ya watu wa Dhimmah na hayo hayakwenda zaidi kwa kile kilichowajibishwa juu yao kuhusiana na Jizyah. Sharia imewaruhusu watu wa Dhimmah kula nguruwe, kunywa ulevi na kuuza wakati yamekatazwa hayo kwa Waislamu na kufanya juu yao kuwa ni kosa linalostahiki adhabu.

Haya ni pamoja na Hukmu nyengine zinazodhihiri katika kutokuwepo fikra ya ndani kuhusiana na uhalisia wao, kutoa haki zaidi kwa Dhimmi kuliko kwa Muislamu. Kwa hakika ni kuwa wanapatiwa haki kwa mujibu wa aina ambayo inapambanishwa juu ya utoaji wa haki hiyo.

Tunaona athari ya hili chini ya Khilafah, wakati baada ya Vita vya Badr, wafungwa wa vita walichagua kubakia na Waislamu kuliko kuregea kwa watu wao (kutokana na namna bora waliyoamiliwa), na huku Wakristo wakiwa upande wa Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Wakiwa ni raia wa Dola ya Kiislamu, walipewa haki na kuhifadhiwa licha ya ukweli kuwa walikuwa wenye dini tafauti.

Kwa kuwa haki za wanaadamu wanapatiwa na Mwenyezi Mungu (swt), zinahifadhiwa na Dola ya Kiislamu, na Dola hiyo itakuja hivi karibuni inshaAllah.

الخلافة_101             #أقيموا_الخلافة#

#ReturnTheKhilafah             #YenidenHilafet                     #TusimamisheniKhilafah

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Fatima Musab
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu