- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Rajab na Suala la Umoja wa Waislamu
(Imetafsiriwa)
Kwa Waislamu wengi leo, neno “Khilafah” huhisika kama jambo la mbali. Baadhi hulihusisha na vitabu vya historia, wengine huliona kama jambo la kindoto au lisilo la kawaida. Hili linaeleweka, hasa kwa kizazi ambacho kimewahi kuishi ndani ya mfumo wa kisasa wa dola ya kitaifa. Lakini kila mwaka, mwezi wa Rajab hutukumbusha kimya kimya mabadiliko makubwa katika historia ya Waislamu. Katika Rajab 1924, Khilafah ilifutwa. Huu haukuwa tu mwisho wa serikali, bali kupotea kwa muundo uliopangilia umoja wa Ummah wa Kiislamu kwa zaidi ya karne kumi na tatu.
Kiini cha Uislamu ni fikra kwamba Waislamu ni Ummah mmoja – jamii moja iliyounganishwa pamoja kwa imani, majukumu, na wajibu wa kimaadili. Hii si majazi au kauli mbiu ya kihisia. Ni kanuni iliyo wazi ya Qur'an. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[إِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ]
“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.” [Qur’an 21:92].
Mwenyezi Mungu (swt) pia anaunganisha umoja moja kwa moja na muongozo na ulinzi:
[وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُواْ] “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.” [Qur’an 3:103].
Wanazuoni wa zamani walielezea kwamba “kamba ya Mwenyezi Mungu” inakusudia Uislamu kama mfumo kamili wa maisha, ikijumuisha utiifu wa pamoja na mamlaka. ‘Abdullah ibn Mas‘ūd (rh) alisema kwamba kamba ya Mwenyezi Mungu ni Jama‘ah — mwili mmoja wa Waislamu.
Kwa hivyo, umoja katika Uislamu kamwe haukukusudiwa kuwekewa mipaka kibinafsi na ya kiroho pekee. Ulikusudiwa kuunda jinsi Waislamu wanavyopanga maisha yao ya pamoja — kisiasa, kijamii, na kiuchumi.
Kwa sehemu kubwa ya historia ya Kiislamu, umoja huu ulikuwa na dhihirisho la kivitendo. Khilafah ilifanya kazi kama mfumo wa kisiasa ambao Waislamu walisimamia haki, usalama, ustawi wa umma, na ulinzi wa pande zote. Haikufuta tamaduni au lugha; utofauti ulikuwepo na ulikubaliwa. Kile kilicho waunganisha Waislamu haikuwa kabila au eneo, bali Uislamu wenyewe.
Mtume (saw) alitilia nguvu fikra hii ya uwajibikaji wa pamoja pale aliposema:
«مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى»
“Waumini, katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao, na kuoneana upole kwao, ni kama mfano wa mwili mmoja: pindi kiungo kimoja kikishtakia maumivu, mwili wote hujibu kwa kukosa usingizi na homa.” (Sahih Muslim)
Khilafah ilipofutwa, Waislamu hawakupoteza imani yao, wala Uislamu ghafla haukuwa na maana. Kilichobadilika ni muundo. Na muhimu zaidi, muundo huo haukubadilishwa na kitu kisichoegemea upande wowote. Njia mpya za kufikiri zilianzishwa ambazo polepole zilibadilisha jinsi Waislamu walivyoelewa kitambulisho, uaminifu, mamlaka, na uwajibikaji.
Utaifa ulikuwa mojawapo ya fikra zenye ushawishi mkubwa zaidi – lakini haukuwa pekee. Utaifa uliwafundisha Waislamu kutanguliza dola ya kitaifa juu ya Ummah, mipaka juu ya udugu, na “maslahi ya kitaifa” juu ya wajibu wa kimaadili.
Sambamba na utaifa, fahamu zengine pia zilibadilisha fikra ya Waislamu. Usekula uliifunga dini kwenye maisha ya kibinafsi. Ubepari ulifafanua upya mafanikio kwa upande wa faida na nguvu. Ubinafsi ulidhoofisha uwajibikaji wa pamoja. Kwa pamoja, fikra hizi zilibadilisha upya ufahamu wa kisiasa wa Waislamu.
Mwenyezi Mungu (swt) anaonya:
[وَلاَ تَكُونُواْ كَالَّذِينَ تَفَرَّقُواْ وَاخْتَلَفُواْ مِن بَعْدِ مَا جَاءهُمُ الْبَيِّنَاتُ]
“Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi.” [Qur’an 3:105].
Matokeo yake ni uhalisia ambao Waislamu wengi wanautambua leo. Kuna hamu kubwa na mshikamano pindi Waislamu wanapokandamizwa — lakini pia hisia chungu ya kutokuwa na msaada. Hii si kwa sababu Waislamu hawajali, bali kwa sababu Ummah umegawanyika.
Ibn Taymiyyah (rh) aliona kwamba kila Waislamu wanapogawanyika, Mwenyezi Mungu aliwaruhusu maadui zao kuwashinda. Inapofahamika katika mwanga huu, Khilafah si ndoto au wito wa vurugu. Badala yake, inawakilisha jaribio la kupangilia maisha ya Waislamu kulingana na maadili ya Kiislamu — hatua kwa hatua, kwa uwajibikaji, na kwa haki ikiwa kiini ndio chake.
Rajab si mwezi wa ukumbusho tu, bali ni wakati wa kutafakari na uwazi. Inawaalika Waislamu kufikiria kwa undani kuhusu umoja — si kama kauli mbiu, bali kama jukumu lililo hai. Kugawanyika kwa Ummah hakukuwa kwa bahati mbaya, na wala hamu ya mshikamano na haki ambayo inaendelea kuishi katika nyoyo za Waislamu. Kama Mwenyezi Mungu (swt) anavyotukumbusha:
[إِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ] “Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.” [Qur’an 21:92].
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Yasmin Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir



