- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Dori ya Magharibi Kafiri katika Kuuchana Umma wetu
na katika Kuivunja Khilafah yetu, Nembo ya Nguvu Yetu
(Imetafsiriwa)
Tulipokuwa Umma mmoja tofauti na mwingine wowote, dola yetu iliweka Rayah (bendera) yake juu ya maeneo yote; ilikuwa mlinzi, kimbilio, na kizuizi dhidi ya yeyote ambaye angeweza hata kufikiria kumshambulia Muislamu mmoja. Waislamu walikuwa mwili mmoja, wakisaidiana kwa ushindi, msaada, na kuimarishana. Iwapo kiungo kimoja kingelalamika, mwili uliobaki ungejibu kwa kukesha na homa. Kisha maadui walielewa kwamba umoja huu na dola hii ndio sababu ya nguvu ya Umma wa Kiislamu na ngao yake ya kinga. Kwa hivyo walianza kulenga ngao hiyo, wakijaribu kuivua, wakifanya juhudi kubwa kwa miaka mingi mirefu hadi walipofikia lengo lao, kwa masikitiko, na kuivunja Dola ya Khilafah mnamo 1924, wakiuchana Ummah wa Uislamu vipande vipande ili kuizuia kurudi katika hali yake ya zamani.
Khilafah haikuanguka ghafla kutokana na mambo ya ndani tu; badala yake, ilivunjwa polepole kupitia mpango mrefu ulioongozwa na dola za kikoloni za Magharibi, huku wasaliti miongoni mwa Waislamu kutoka Waarabu na Waturuki wakati huo, ambao waliathiriwa na miito yao ya utaifa, utengano, na mengineyo. Hivyo, uvunjaji huo ulikuwa wa kifikra na kisiasa kabla haujawa wa kijeshi.
Sifa kuu za mpango huo zilikuwa:
- Kudhoofisha fikra ya Kiislamu miongoni mwa Waislamu kupitia uvamizi wa kifikra, kupotosha Uislamu, na kupanda fikra za utaifa ili kuvunja umoja wa Ummah na kuhamisha utiifu kutoka kwa Uislamu hadi kwa rangi na nchi.
- Kupanua ushawishi wa kisiasa usio wa moja kwa moja katika hatua ya awali kupitia madeni na kuingilia uteuzi na kufukuzwa kwa masultani.
- Kuvunja rasmi Khilafah.
- Kugawanya ardhi za Waislamu baadaye katika dola bandia na kuchora mipaka kwa lengo la kuwazizuia kuungana tena.
- Kugawanya zaidi kile ambacho tayari kilikuwa kimegawanyika na kuendelea kuchochea vita na hisia za kimadhehebu na za utaifa.
Yeyote anayechunguza kwa makini historia ya Dola ya Kiislamu anatambua dori kubwa ya Magharibi katika kile kilichotokea. Hii haimaanishi kwamba tunakataa mapungufu ya Makhalifa, wanazuoni, na Ummah katika kushindwa kujizatiti kwa njia zinazoweza kurudisha nyuma njama za maadui. Badala yake, hapa tunatafuta kutoa mwanga zaidi kuhusu udanganyifu mkubwa wa Magharibi na dori yake kubwa katika kile kilichotokea, ili kuelewa ukubwa wa walichofanya, kuchukua mazingatio, na kuinuka tena kwa kuzuia mipango yao yote.
Magharibi kafiri ilianzisha vita vikali dhidi ya fikra za Uislamu, kiasi kwamba ni nadra fahamu au utawala wowote wa Kiislamu uliepuka upotoshaji, mkanganyiko, na uzushi. Kutokana na udhaifu wa ufahamu katika zama za baadaye kuhusu Khilafah, wanazuoni hawakusimama kukabiliana na shambulizi hili kwa nguvu za kutosha, jambo ambalo lilisababisha kupenya kwa fahamu za Kimagharibi na sheria za Ulaya—mwanzoni kwa msingi kwamba hazikugongana na Uislamu na ziliendana nao—na kusababisha, baadaye, kuenea kwa fikra za Kimagharibi na masuluhisho yake, na kimya kuhusu hilo.
La kusikitisha yote yaliambatana na udhaifu wa Khilafah katika miaka yake ya mwisho na ongezeko la utekelezaji mbaya ndani yake. Haikuwa tena dola ile iliyotabikisha kanuni ya Kiislamu na kuibeba kwa nguvu, kutokana na udikteta wa baadhi ya makhalifa, utawala dhaifu, kupenya kwa ushawishi wa kigeni, na kufungwa kwa maamuzi ya kisiasa kupitia madeni ya nje, pamoja na kushuka kwa sekta ya viwanda na umakini kwa sayansi, miongoni mwa mambo mengine. Wala hatupaswi kusahau kushindwa kwa dola kupata silaha za hali ya juu na uzembe wake katika suala hili, ambao ulisababisha kurudi nyuma kwa kiasi katika vifaa vyake vya kijeshi ikilinganishwa na dola zengine, na kusababisha kushindwa mara nyingi na mwanzo wa kufifia kwa taswira ya dola isiyoshindika.
Kwa upande mwingine, Magharibi ilifanikiwa kujionyesha kama mshindi mkuu ambaye sheria na maagizo yake lazima yafuatwe na ulimwengu.
Maadui hawakuishia hapo; badala yake, waliwageukia wasaliti miongoni mwa Waarabu na Waturuki, wakiwaajiri kuongoza harakati za kujitenga na kutenda kama walinganizi wa utaifa, uzalendo, usekula, na Uenezaji wa Umagharibi, na hivyo kuzidisha hali hiyo na kuongeza udhaifu juu ya udhaifu. Mustafa Kemal alikuwa mmoja tu wa wasaliti hawa waliokubali kuwa chombo cha ubomoaji mikononi mwa maadui, ambao kupitia wao walivunja jengo kubwa la Khilafah na kulibadilisha na dola ya kitaifa ambayo baadaye ilikubali mgawanyiko wa Ummah wa Kiislamu.
Kwa kuanguka kwa Khilafah, Ulaya—inayoongozwa na Uingereza—iliushukia Ummah wa Uislamu kama walaji wanaoshuka kwenye sahani zao, wakiendeleza kile walichokuwa wameanzisha cha mgawanyiko na ukoloni kabla ya kuvunjwa kwake. Walihitimisha makubaliano kama vile Mkataba wa Sykes-Picot na mengineyo, walichora mipaka, wakaweka vizuizi, na kuweka ulinzi juu ya kila kitambaa, ambacho amri zake zilikuwa mikononi mwa mabwana zake.
Kwa sababu hiyo, Palestina ilikaliwa kimabavu na kubaki hivyo hadi leo, ikilalamika kuhusu usaliti wa wasaliti na uzembe wa wazembe, na kulipia gharama ya mgawanyiko na kutokuwepo kwa dola. Mwenyezi Mungu amrehemu Khalifah Abdul Hamid, ambaye alizuia unajisi wake hadi pumzi yake ya mwisho. Kauli yake bado inasikika kwa sauti kubwa masikioni mwetu: “Endapo Dola ya Khilafah itachanwa, basi wataweza kuichukua Palestina bila thamani. Lakini maadamu niko hai, kisu cha daktari wa upasuaji kuchonichoma mwilini ni sahali kwangu kuliko kuona Palestina ikikatwa kutoka kwa Dola ya Kiislamu. Hili halitakuwa hivyo; siwezi kukubali kukatwa kwa miili yetu wakati tuko hai.”
Ndiyo, cha kusikitisha tumepitia kukatwa kwa miili yetu huku tukiwa hai. Kile ambacho ndugu zetu nchini Palestina wanaendelea kuteseka leo sio tofauti na ambayo Waislamu kila mahali wameteseka kutokana na ukoloni. Orodha ya majeraha yanayovuja damu ya Ummah wetu ni ndefu—kuanzia Kashmir hadi Chechnya, kuanzia Turkestan hadi Timor Mashariki hadi Myanmar, na zaidi.
Kwa hivyo je, Magharibi imeridhishwa na yote ambayo imeyafanya? Bila shaka hapa. Badala yake, inaendelea kutumia juhudi zake zote kuzuia kurudi kwa Khilafah. Amerika imekuwa stadi wa kugawanya zaidi kile ambacho tayari kimegawanyika na kuchochea hisia za kimadhehebu na za kitaifa wakati wowote inapoweza. Hali za Yemen, Sudan, Syria, na kwengineko leo hazifichiki kwa mtu yeyote.
Enyi Waislamu: nyinyi ni Umma mmoja tofauti na mwingine wowote. Umoja wenu na Khilafah yenu vilikuwa sababu ya nguvu yenu, mwamko wenu, na radhi ya Mola wenu Mlezi pamoja nanyi. Ndiyo maana Magharibi mkoloni kafiri iliivunja. Kwa hivyo je, hamtakunja mikono ya mashati ya azma yenu ya kurudi jinsi mlivyokuwa hapo awali—Umma mmoja wenye dola moja na bendera moja—ili kuwakasirisha maadui zenu? Je, nyoyo zenu hazitamani kuregesha heshima na izza yenu, kutakasa Aqsa yenu na Ka‘bah yenu, na kuwanusuru ndugu zenu wanaokandamizwa kila mahali?
Hakika, kufanya kazi ya kuregesha Khilafah ni heshima ya dunia hii na Akhera. Kupitia hiyo pekee mtapata tena uongozi wenu, kuhifadhi umoja wenu, na hata kuokoa ulimwengu mzima kutokana na dhulma, udhalimu, na shimo ambalo umeshukia. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللهِ]
“Na siku hiyo Waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu” [Ar-Rum: 4–5].
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Minnatullah Taher



